231011 Euro Gipfel
24 Oktoba 2011Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa walifanya bidii ya kuonyesha umoja kwenye mkutano huo. Ujumbe uliowasilishwa na viongozi hao ni msimamo wa pamoja katika kulitafuta suluhisho la mgogoro wa madeni. Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanaelekea kuwa wamepiga hatua katika juhudi zao za kuukabili mgogoro mkubwa wa madeni.
Katika juhudi za kuepusha mfarakano, Rais Sarkozy amekiri kwamba amelazimika kurudi nyuma katika mabishano yake na Ujerumani juu ya jinsi ya kuchangia katika mfuko wa kuziokoa nchi zilizolemewa na madeni katika Umoja wa Sarafu ya Euro.
Hapo awali kiongozi huyo wa Ufaransa alipendekeza kuugeuza Mfuko huo kuwa benki na kuiwezesha wakati wote kukopa kutoka Benki Kuu ya Ulaya (ECB).
Viongozi wa Umoja wa Ulaya na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Fedha la Kimataifa, Christine Lagard, wamesifu hatua nzuri iliyopigwa kwenye mkutano huo.
Hata hivyo, marais na mawaziri wakuu hawakufikia maamuzi thabiti kwenye mkutano wao wa mjini Brussels.
Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, amekiri kwamba hajui ni suluhisho lipi litakalokuwa mujarabu.
"Kwa usemi mwingine, miongoni mwa wataalamu wote waliokuwapo, hakuna anayeweza kusema kwa uhakika njia gani, ni sahihi kwa asilimia 100, kwa sababu tumeingia katika mazingira tusiyoyajua. Kwa sababu, hali kama hiyo katika Umoja wa Sarafu kama wa eneo la Euro, haijawahi kutokea." Amesema Kansela Merkel.
Viongozi wa Umoja wa Ulaya wameahidi kutoa maelezo ya undani zaidi kwenye mkutano wao mwingine utakaofanyika Jumatano ijayo.
Rais Sarkozy na Kansela Merkel wamesisitiza kwamba baina yao kwa jumla pana makubaliano.
Katika hatua nyingine ya juhudi za kuukabili mgogoro wa madeni, viongozi hao Ujerumani na Ufaransa waliwasilisha ujumbe kwa Waziri Mkuu wa Italia, Silvio Berlusconi, kwamba ili masoko ya fedha yaanze tena kuzinunua dhamana na ili kurejesha hali ya uhakika katika eneo la Euro, Italia itapaswa ifanye mageuzi zaidi ya kiuchumi.
"Tunaendelea kuwa na imani na hisia za uwajibikaji wa wanaisasa, na wanaopitisha maamuzi ya kifedha na kiuchumi nchini Italia." Amesema Rais Sarkozy.
Viongozi wa Umoja wa Ulaya wana wasiwasi huenda kiasi cha Euro bilioni 440 hakitatosheleza kwa ajili ya kuiokoa nchi kubwa kama Italia. Hata hivyo, Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Jose Manuel Barosso amesema kazi inaendelea kufanyika na maamuzi yanatarajiwa kupitishwa Jumatano. Barroso amesema ana imani kwamba maamuzi hayo yatapitishwa.
Mwandishi: Riegert, Bernd/ZR Tafsiri: Abdu Mtullya Mhariri: Mohammed Khelef