Scholz amuonya von der Leyen kuhusu vyama vya itikadi kali
25 Mei 2024Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amemuonya Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen, kutojaribu kutafuta muhula wa pili madarakani baada ya uchaguzi wa bunge la Ulaya, kwa msaada wa vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia.
Scholz amesema ni wazi kuwa uundwaji wa halmashuri kuu ijayo haupaswi kutegemea wingi wa bungeni unaohitaji uungaji mkono wa wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia, na kuelezea masikitiko yake juu ya utata wa baadhi ya matamko ya kisiasa yaliosikika hivi karibuni.
Soma pia:Wahafidhina Ulaya kumuidhinisha von der Leyen muhula wa pili
Mnamo mwezi Aprili von der Leyen alikataa kuondoa uwezekano wa kushirikiana na kundi la wahafidhina wa mrengo wa kulia na wanamageuzi, ECR, ambalo linahusisha chama cha waziri mkuu wa Italia Georgina Meloni cha Brothers of Italy.
Von der Leyen alitetea uamuzi wake katika bunge la Ulaya siku ya Alhamisi, akisema alishirikiana vyema na Georgina Meloni katika Baraza la Ulaya kama ilivyokuwa na wakuu wengine wa nchi na serikali.
Scholz amesema msimamo wake wa wazi ni kwamba itawezekana tu kuunda urais wa halmashauri kuu kupitia vyama vya jadi, na jambo lolote lingine litakuwa kosa kwa mustakabali wa Ulaya.