Scholz ayaainisha malengo yake bungeni kama kansela
15 Desemba 2021Hotuba ya kwanza ya Olaf Scholz bungeni tangu alipochukua usukani kutoka kwa mtangulizi wake aliyestaafu Angela Merkel wiki iliyopita ilijikita zaidi katika masuala ya ndani. Alisisitiza haja ya dharura ya kupambana na janga la Corona na mpango wa muda mrefu wa kuboresha masuala ya uchumi na jamii.
Kansela Olaf Scholz atoa zingatio kwa Ulaya katika ziara yake ya kwanza
Olaf mwenye umri wa miaka 63, ambaye tayari amezuru Paris, Brussels na Warsaw tangu alipopokezwa mikoba, pia aligusia umuhimu wa kuuimarisha Umoja wa Ulaya, ili kusimama katika nafasi sawa na washirika kutoka chi za Atlantiki mnamo wakati kuna vitisho dhahiri, mfano Urusi kurundika wanajeshi katika mpaka wake na Ukraine.
Olaf Scholz aapishwa kuwa Kansela wa Ujerumani
Scholz amesema ajenda atakayoipa kipaumbele ni kudhibiti janga la COVID-19, huku akiwahimiza watu kupokea chanjo.
“Leo ninawaambia watu wa nchi hii kwamba ndiyo mambo yataimarika. Ndiyo tutashiriki kwa nguvu zote katika vita dhidi ya janga la COVID na tutaishinda hali hii tete," amesema Scholz.
Juhudi za kupambana na athari za mabadiliko ya tabia nchi
Kansela huyo mpya amesema wamesalia na miaka 23 ili kutokomeza kabisa matumizi ya nishati zinazochafua hewa. Jambo ambalo alisema litamaanisha mageuzi makubwa ya kiviwanda na kiuchumi katika kipindi cha miaka 100 ijayo.
Scholz alihudumu kama naibu kansela na vilevile waziri wa fedha katika serikali ya Merkel katika miaka minne iliyopita. Lakini amesema serikali yake mpya ya muungano kwa ushirikiano na chama cha watetezi wa mazingira na wanaopendelea biashara (Free Democrats) itakuwa ‘mwanzo mpya'.
Amesema Ujerumani inapaswa kuongeza juhudi za kuzalisha nishati mbadala zisizochafua hewa ifikapo mwaka 2030. Lakini pia itanue miundo mbinu yake mfano kuongeza vituo vya ‘kuchaji' magari yanayotumia umeme.
Serikali yake pia itaweka mpango wa uwekezaji kwa mfano kutanua juhudi za mabenki kuwasaidia wawekezaji wanaochipuka.
Scholz amesisitiza kuwa mageuzi kama hayo yanaweza tu kufikiwa ikiwa kutakuwa na mshikamano wa kijamii akigusia pia mipango ya kuongeza mishahara ili kuwepo usawa.
Upinzani wakosoa mipango ya mikopo zaidi
Upinzani ulielekeza ukosoaji wao kuhusu pendekezo la serikali hiyo mpya kuchukua mkopo zaidi kufadhili miradi mipya ya uwekezaji. Wanasiasa wa mrengo wa shoto wameikosoa serikali ya Scholz kwa sera ya kuwatoza mabwenyenye ushuru wa juu. Wale wa siasa za mrengo wa kulia wamekosoa sera ya serikali ya Scholz ya kifedha isiyo endelevu.
Kuhusu sera ya kigeni alisema ufanisi wa Umoja wa Ulaya ni kipaumbele cha Ujerumani na serikali yake itafanya kazi kuuimarisha umoja huo.
Scholz anatarajiwa kuhudhuria mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya kwa mara ya kwanza Alhamisi kama kansela wa Ujerumani.
(RTRE)