Scholz azitaka Kosovo na Serbia kutafuta amani
10 Juni 2022Kansela Scholz ambaye yuko nchini Kosovo kuanza ziara ya mataifa kadhaa ya kanda ya Balkan, amesema vita ya Urusi nchini Ukraine imefanya suala la utulivu wa eneo hilo kuwa muhimu zaidi.
Katika mkutano wa pamoja wa habari na waziri mkuu wa Kosovo, Albin Kurti, Kansela Scholz amesema majadiliano yanahitaji mtazamo wa kujenga, na kuongeza kuwa makubaliano ya mwisho yatachangia kuongeza utulivu kwenye kanda ya Balkan Magharibi.
Soma pia: Baerbock aonya dhidi ya ushawishi wa Urusi ziarani Balkan
Mazungumzo ya kusuluhisha yanayowezeshwa na Umoja wa Ulaya ambayo yalianza miaka 11 iliyopita, yamekuwa na athari ndogo, na mvutano kati ya mahasimu hao wa zamani wa kivita unaendelea.
Kansela wa Ujerumani amesema kwamba katika wakati ambapo ukaliaji wa Urusi nchini Ukraine ukiendelea, utatuzi wa suala la Kosovo na Serbia unageuka hata muhimu zaidi.
"Katika nyakati kama huu, thamani ya usalama na uhuru inakuwa dhahiri zaidi kwetu. Ni sababu kubwa na muhimu hata zaidi kwamba Kosovo na Serbia zinatafuta suluhisho la kisiasa linalochangia utulivu wa kikanda," alisema Scholz.
Soma pia: Shirika la Frontex lakiuka haki za binadamu eneo la Balkan?
Kansela pia ameziomba serikali za Serbia na Kosovo kutatua suala la utambuzi wa Kosovo, kwa sababu haifikiriki kwamba nchi mbili zisizotambuana zinaweza kuwa wanachama wa Umoja wa Ulaya.
Kosovo ambayo ni jimbo la zamani Serbia, ilitangaza uhuru wake mwaka 2008, muongo mmoja baada ya vita vya kikatili vya mwaka 1998 hadi 1999 kati ya waasi waliotaka kujitenga wa asili ya Albania na vikosi vya Serbia.
Vita hivyo vilimalizika baada ya kampeni ya siku 78 ya mashambulizi ya anga ya jumuiya ya kujihami NATO iliyowafurusha wanajeshi wa Serbia na kukiingiza kikosi cha kulinda amani.
Utambuzi wa uhuru wa Kosovo
Mataifa mengi ya magharibi yameutambua uhuru wa Kosovo, lakini Serbia na washirika wake Urusi na China hawajaitambua.
Mataifa sita ya kanda ya Balkan yako kwenye ngazi tofauti za maombi yao ya kujiunga na Umoja wa Ulaya.
Serbia na Montenegro zimeanza majadiliano kamili, huku Albania na Macedonia Kaskazini zikikabiliwa na uchelewaji ndani ya Umoja wa Ulaya kuanzisha mazungumzo yao.
Kosovo na Bosnia zimo katika hatua za mwanzo za mchakato wa uanachama. Waziri Mkuu wa Kosovo Albin Kurti amesema nchi yake itaomba hadhi ya mgombea wa uanachama wa Umoja wa Ulaya, jambo ambalo Ukraine, Moldova na Georgia zimefanya.
Soma pia: Serbia na Kosovo waridhia shinikizo la Berlin na Paris
Kansela Scholz amesifu hatua ya Kosovo kuunga mkono vikwazo vya umoja wa Ulaya dhidi ya Urusi, na kuisifu serikali mjini Pristina kuwa mshirika wa kutegemewa, huku akiikumbusha Serbia, ambayo haijaunga mkono hatua ya vikwazo kuwa nchi yoyote inayotaka kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya inapaswa kusimamia sheria na desturi za umoja huo.
Scholz anapanga pia kuzitembelea Serbia, Ugiriki, Macedonia Kaskazini na Bulgaria, wakati wa ziara yake ya Balkan.
Chanzo: Mashirika