Senegal: Utulivu warejea baada ya maandamano yenye ghasia
6 Juni 2023
Waziri wa mambo ya ndani wa Senegal, Antoine Felix Diome, akitoa tathmini ya yaliyojiri wakati wa maandamano amesema nchi hiyo imevamiwa na alichokiita, ''nguvu za kimiijuza'' akimaanisha makabiliano baaina ya waandamanaji na vyombo vya usalama, ambayo yalisababisha vifo vya watu 16, na kujeruhi wengine zaidi ya 30.
Soma pia: UN na AU zahimiza amani kufuatia machafuko Senegal
Duru za polisi zimesema kuwa watu wapatao 500 walikamatwa katika maeneo yote ya nchi. Mkurugenzi wa kitengo cha usalama wa taifa la Senegal Ibrahima Diop, ametoa ufafanuzi.
''Wengi wa waliokamatwa katika tukio hili ni watu hatari wenye silaha. Hadi sasa wanafika 500, miongoni mwao wakiwemo watoto na wenye uraia wa kigeni, amesema Diop na kuongeza kuwa ''sehemu kubwa ya waliokamatwa ni wale waliokutwa na mabomu ya petroli, na vifaa vyenye ncha kali, na silaha za moto.''
''Maafisa wa usalama walikabiliana na waandamanaji wenye fujo, ambao haja yao haikuwa kuelezea maoni yao, bali kufanya vitendo vya hujuma'', alidai afisa huyo.
Maoni mchanganyiko miongoni mwa raia wa Senegal
Matamshi hayo ya mkurugenzi wa kitengo cha usalama wa taifa yamezua maoni mchanganyiko katika umma wa Senegal.
Biram Bass ni mwanachama wa asasi ya kiraia mjini Dakar, na amepinga vitendo vya vurugu. Anasema hakuna anayenufaika kutokana na ghasia iliyosababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali, na kuongeza kuwa hali hiyo ingeweza kuepukika.
Soma pia: Guterres alaani vurugu za Senegal
Rais wa Senegal hapo jana aliitisha kikao cha dharura cha kamati kuu ya chama chake cha Alliance for Republic, agenda kuu ikiwa kujadili mikakati ya kuumaliza mgogoro huu.
Wachambuzi wasema hii ni afueni ya muda tu
Ingawa hali ya utulivu imerejea, mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Musa Diaw anadhani shida bado ipo.
''Hawa ni watu wasio na kazi, hii ni njia ya kuelezea malalamiko yao hadharani kwa sababu kuna manung'uniko katika jamii kuhusu namna nchi inavyotawaliwa na wanasiasa walioko madarakani,'' alisema Diaw.
Umati wa waandamanaji uliokuwa umekusanyika katika viwanja vya uhuru mjini Dakar ulihanikiza kauli mbiu isemayo, ''kupambana dhidi ya ukandamizaji ni wajibu wa kila raia.'' Mnamo siku chache zijazo itajulikana ikiwa vuguvugu hili la upinzani litaendelea au litasita nchini Senegal.
Kiini cha mivutano hii ya karibuni ni hukumu ya kifungo cha miaka miwili jela iliyotolewa dhidi ya kiongozi wa upinzani Ousmane Sonko, kwa kukutwa na hatia ya ''kuwachochea vijana.''