Serikali ya DRC yazuia vifaa vya mawasiliano vya Ulaya
5 Desemba 2023Vyanzo kadhaa vya habari vimeliambia shirika la habari la AFP, kwamba Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ilikataa kuruhusu vifaa vya vya mawasiliano ya Satalaiti vya tume ya Umoja wa Ulaya kuingizwa nchini humo kutokana na khofu kwamba vifaa hivyo vingetumika kubadilisha matokeo ya uchaguzi wa rais baadae mwezi huu. Vifaa vilivyozuiwa na serikali ya Kongo ni pamoja na simu na vifaa vya urahisishaji mawasiliano ya mtandao pamoja navifaa vya ufuatiliaji safari za magari, ili kuwarahisishia waangalizi kuwasiliana na timu yao ya uongozi mjini Kinshasa. Umoja wa Ulaya ulichukuwa hatua ya ghafla Novemba 26 ya kufuta ujumbe wake wa uangalizi wa uchaguzi wa Kongo ikisema imetokana na sababu za kiufundi. Hata hivyo maafisa chungunzima wameliambia shirika la habari la AFP kwamba hatua ya Umoja wa Ulaya imechukuliwa baada ya ombi lake la muda mrefu la kutaka kibali kwaajili ya kuingiza vifaa vyake kukataliwa.