Shambulio lapiga Beirut Kusini baada ya ilani ya Israel
16 Novemba 2024Tangu Jumanne, Israel imefanya mashambulio kadhaa katika vitongoji vya kusini mwa mji huo, ambao ni ngome ya Hezbollah. Picha za vidio za shirika la habari la AFP zimeonyesha moshi ukitanda juu ya majengo hayo Jumamosi asubuhi.
Msemaji wa jeshi la Israeli, Avichay Adraee, aliwataka wakaazi wa kitongoji cha Haret Hreik kuhama kabla ya shambulio, akionya kuwa eneo hilo ni karibu na miundombinu ya Hezbollah.
Soma pia: Israel yashambulia kusini mwa Beirut usiku kucha
Mashambulio ya anga ya mara kwa mara ya Israeli yamesababisha idadi kubwa ya raia kukimbia kusini mwa Beirut, huku wengine wakirudi mchana ili kukagua nyumba na biashara zao.
Pia, katika eneo la kusini mwa Lebanon, Israel ilifanya mashambulio kadhaa Ijumaa usiku na Jumamosi asubuhi, huku Hezbollah ikidai kushambulia kambi ya jeshi la Israel.
Mamlaka za Lebanon zinasema watu zaidi ya 3,440 wameuawa tangu Oktoba mwaka jana kutokana na vita hivyo, huku hasara ya kiuchumi ikifikia zaidi ya dola bilioni 5.