Silaha za sumu zilitumiwa Syria
13 Desemba 2013Wakaguzi hata hivyo wamesema hawakuweza kuthibitisha matumizi ya silaha katika maeneo mawili kati ya saba yaliyokaguliwa, na kwa sababu ya mamlaka yenye kikomo walio nayo, hawakusema ni nani alihusika na mashambulizi hayo.
Ripoti hiyo imesema ushahidi umeonyesha kuwa silaha za sumu huenda zilitumika katika eneo la Khan al Assal nje ya mji wa Aleppo, Jobar, viungani mwa Damascus, Saraqueb, karibu na mkoa wa Idlib katika upande wa kaskazini mashariki na Ashraffiah Sahnaya nje ya mji wa Damascus. Katika matukio mawili, ilipata “dalili za sumu ya Sarin”.
Serikali na upinzani zilishutumiana kila mmoja kwa matumizi ya silaha za sumu katika maeneo hayo.
Katika ripoti ya mwanzo, iliyotolewa Septemba 16, kikundi hicho kinachoongozwa na Ake Sellestrom kilisema kuwa ushahidi uliokusanywa katika eneo la Ghouta mjini Damascus kufuatia shambulizi la Agosti 21 ulithibitisha wazi kuwa makombora ya nchi kavu yenye gesi ya Sarin yalitumiwa”.
Hali hiyo ilizifanya Marekani na Urusi kukubaliana kuhusu namna ya kuziangamiza silaha zote za Syria ifikapo katikati ya mwaka wa 2014. Mchakato wa kuziondoa silaha za sumu nchini Syria unaendelea kwa sasa.
Wakaguzi wa Umoja wa Mataifa wamesema vipimo vya damu vilivyokusanywa na serikali ya Syria na kuthibitishwa na Umoja wa Mataifa kwa kutumia mbinu za vinasaba, “vilionyesha dalili za sumu ya sarin”.
Ripoti hiyo imesema Jopo la uchunguzi la Umoja wa Mataifa halikuweza kuyatembelea maeneo yote ambayo silaha za sumu zilidaiwa kutumika, kwa sababu ya mazingira duni ya usalama. Kati ya maeneo saba yaliyotajwa kwenye ripoti hii ya mwisho, kundi hilo lilizuru tu Ghouta na Jobar.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon atalihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hii leo kuhusiana na ripoti hiyo, na kisha Baraza la Usalama siku ya Jumatatu. Wakati huo huo Shirika la kutetea haki za binaadamu la Amnesty International limewakosoa viongozi wa Ulaya likisema wanapaswa “kuinamisha vichwa vyao katika aibu” kuhusiana na namna wanavyowashughulikia wakimbizi wa Syria wanaotoroka mapigano nchini mwao.
Katika ripoti yake, shirika hilo linasema nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya zimetoa karibu nafasi 12,000 pekee kwa wakimbizi wa Syria kama sehemu ya lengo la Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwashughulikia Wakimbizi la kutoa nafasi 30,000. Katibu Mkuu wa Amnesty International Salil Shetty amesema Umoja wa Ulaya umeshindwa kabisa kutekeleza jukumu lake katika kuwapa makao wakimbizi ambao wamepoteza kila kitu isipokuwa tu maisha yao, na idadi ambayo umoja huo umejiandaa kuwashughulikia ni ya kutia huzuni. Kati ya nafasi 12,000 zilizotolewa, 10,000 zimeahidiwa na Ujerumani. Ufgaransa imetoa nafasi 500 wakati Uhispania ikiwa na 30.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Daniel Gakuba