Sudan Kusini yaahirisha uchaguzi mkuu hadi 2026
14 Septemba 2024Serikali ya Sudan Kusini imesogeza mbele uchaguzi mkuu hadi Disemba mwaka 2026, kutokana na kile Ofisi ya Rais inachosema ni "changamoto mbalimbali za kiusalama" zinazoikabili nchi hiyo.
Tangazo hilo lililotolewa na Ofisi hiyo kupitia mtandao wa Facebook lilisema Rais Salva Kiir ametangaza kuongeza muda huo wa mpito kwa miaka miwili pamoja na kuahirisha uchaguzi uliopangwa Disemba mwaka huu hadi Disemba 22, mwaka 2026.
Soma zaidi. Mswada wa usalama Sudan Kusini sheria bila saini ya rais
Sudan Kusini imekuwa katika aina fulani ya utulivu tangu makubaliano ya 2018 yaliyomaliza mzozo wa miaka mitano uliosababisha vifo vya maelfu ya raia, lakini vurugu kati ya jamii hasimu bado hutokea mara kwa mara.
Kabla ya tangazo hilo kutolewa, Sudan Kusini ilikuwa inapanga kuchagua viongozi wa kurithi serikali ya mpito ya sasa inayoongouzwa na Salva Kiir na Makamu wa Kwanza wa Rais Riek Machar, ambao vikosi vyao vilipigana wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe.