UNICEF: Watoto mil 400 duniani wanapitia ukatili majumbani
11 Juni 2024Takwimu hizo za UNICEF zimekusanywa kutoka katika mataifa 100 kuanzia mwaka 2010 hadi 2023 na zilijumuisha aina zote za ukatili ikiwemo "adhabu za kimwili" na dhuluma za kisaikolojia.
Shirika hilo linafasili ukatili wa kisaikolojia kuwa unajumuisha maneno ya kutwezwa kwa mtoto ikiwemo kuwapa majina yanayochukiza kwenye jamii, wakati ukatili wa kimwili ukiainishwa kuwa ni pamoja na matendo yoyote yanayokusudiwa kusababisha maumivu ya kimwili au usumbufu, bila majeraha.
Shirika hilo limesema kati ya watoto hao milioni 400 ulimwenguni, milioni 330 wanapitia ukatili wa kimwili.
Soma pia:Kesi hatarishi kwa ustawi wa watoto zimeongezeka Ujerumani
Ripoti hiyo imeongeza kwamba licha ya nchi nyingi zaidi kupiga marufuku adhabu ya viboko kwa watoto, karibu watoto milioni 500 walio chini ya umri wa miaka mitano hawajalindwa kisheria dhidi ya vitendo hivyo.
Rpoti hiyo inaonesha kuwa jamii nayo inaamini juu ya adhabi za kimwili, kwani mtu mzima mmoja anaewajibika kwa mtoto kati ya wanne anaamini kwamba adhabu za kimwili ni muhimu ili kuwarekebisha ipasavyo watoto wao.
Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Catherine Russell amesema watoto wanapopitia aina hiyo ya ukatili inaweza kuchochea kupungua kujiamini kwao na maendeleo yao kwa ujumla na kupoteza hisia ya kutojithamini.
Kuadhimishwa siku ya kucheza duniani
Kwa mara ya kwanza UNICEF imechapisha matokeo ya utafiti wao kuhusu fursa ya watoto kucheza katika kuadhimisha kwa mara ya kwanza siku ya kimataifa ya kucheza ambayo itakuwa ikiadhimishwa Juni 11.
Kulingana na takwimu kutoka nchi 85, mtoto mmoja kati ya wawili walio na umri wa miaka minne hawezi kucheza na mlezi wao nyumbani, na takriban mtoto mmoja kati ya wanane walio chini ya umri wa miaka mitano hana midoli ya kuchezea kabisa.
Takriban asilimia 40 ya watoto wenye umri wa miaka miwili hadi minne hawana muingiliano wa kihisia wanapokuwa nyumbani, na mmoja kati ya watoto kumi hana uwezo wa kufikia shughuli muhimu katika kukuza maendeleo ya utambuzi, kijamii, na kihisia, kama vile kusoma, kusimulia hadithi, kuimba na hata kuchora.
Soma pia:UN: Ukatili dhidi ya watoto waongezeka pakubwa 2020
Baadhi ya wazazi waliozungumza na DW Kiswahili wanasema, maendeleo ya teknolojia, mbio za kusaka maisha bora ni miongoni mwa sababu zinawafanya wazazi wengi kutokutenga muda wa kucheza na watoto wao.
Unicef imesema katika siku hii ya kucheza inayoadhimishwa kwa mara ya kwanza , lazima jamii iungane na kujizatiti kwa mara nyingine ili kukomesha ukatili dhidi ya watoto na kuchechemua malezi chanya miongoni mwa watoto na uchezaji wenye tija.