Somalia:Takriban watu 100 wameuawa katika milipuko ya mabomu
30 Oktoba 2022Tukio hilo liliendeshwa hapo jana katika mtaa wenye shughuli nyingi mjini Mogadishu. Kuliwahi kutokea shambulio katika eneo hilo miaka mitano iliyopita ambapo lori lililojazwa vilipuzi lilisababisha vifo vya zaidi ya watu 500.
Rais Mohamud akiwa kwenye eneo kulikotokea milipuko hiyo, aliwaambia waandishi wa habari kuwa karibu watu wengine 300 walijeruhiwa huku akiwaomba washirika wa kimataifa kuwaagiza madaktari nchini humo na kusema hawawezi kuwasafirisha majeruhi wote nje ya nchi kwa matibabu.
Kundi la al-Shabab lenye mafungamano na al-Qaida ambalo hushambulia zaidi mji mkuu Mogadishu na ambalo linadhibiti eneo kubwa ya nchi hiyo, limedai kuhusika na shambulizi hilo na kusema lililenga ofisi za wizara ya elimu ambayo wametaja ni ngome ya maadui wanaopokea msaada kutoka katika nchi zisizo za kiislamu ili kuwaondoa watoto wa kisomali katika imani ya Kiislamu.