Tanzania yaanza utoaji chanjo ya Corona kitaifa
3 Agosti 2021Kampeni hiyo ya kitaifa imeanza kwa kutolewa chanjo kwa makundi yaliyopewa kipaumbele yakijumuisha watumishi wa afya, viongozi na hata waandishi wa habari.
Watu wameendelea kujitokeza katika vituo mbalimbali ambavyo vimetambuliwa na serikali kwa ajili ya kutoa huduma hiyo muhimu kwa dunia ya sasa, wakiwemo wanasiasa, wahudumu wa afya na familia za viongozi mbalimbali. Muitikio huu wa watu wa tabaka la juu unatajwa kuchangiwa na kujiridhisha kwao kwamba kuna umuhimu wa kupata chanjo hiyo ili kuwa katika dunia ilio salama bila hofu ya corona na kuwawezesha kufanya shughuli zao kwa uhuru.
Soma pia:Rais Samia azindua chanjo ya COVID-19 Tanzania
Baadhi ya wanasiasa ambao wamefika katika vituo vya kutolea huduma wamesifu mchakato na utaratibu wa utolewaji wa chanjo hiyo, kwa hoja kwamba mbali na elimu walioipata kabla, huelimishwa tena na kutolewa fursa ya kuuliza maswali ili kujiridhisha kabla ya kufikia hatua ya uchomaji wa chanjo hiyo aina ya kampuni ya Johnson Johnson.
Mwenyekiti wa chama cha NCCR Mageuzi James Mbatia ambae ameambatana na mkewe pamoja na viongozi wengine wa chama katika hospitali ya Agha Khan ili kupata chanjo hiyo, punde baada ya kuchanja, amewaambia wanahabari uhitaji wa huduma hiyo bado ni mkubwa hivyo kuna haja ya serikali kuruhusu sekta binafsi iwekeze katika huduma hiyo ili kundi kubwa la watu wenye uhataji wapate chanjo: Kampeni ya kupambana na janga la Covid-19 nchini Tanzania inaendelea kukabiliana na changamoto lukuki, ikiwemo upinzani dhidi ya chanjo unaochochewa na taarifa za upotoshaji kuhusu madhara ya chanjo hizo, zinazoenezwa kupitia mitandao ya kijamii, huku baadhi ya raia wakionesha mashaka hata kuhusu ugonjwa huo wakiamini ni njama za mataifa ya Magharibi kupunguza idadi ya watu katika mataifa maskini.
Soma pia: Tanzania, Rwanda kushirikiana mapambano dhidi ya Covid-19
Katika kujaribu kujibu maswali na wasiwasi unaooneshwa na wananchi kuhusu ugonjwa wa Covid-19, wizara ya afya kupitia mamlaka ya dawa na vifaa tiba, TMDA, imetoa waraka wenye kurasa tisa ukifafanua kuhusu ugonjwa huo, ambapo pia imeelezea aina za chanjo za Corona na namna zinavyofanya kazi, faida za kuchanja, waraka ambao utakwenda sambamba na ufafanuzi wa wataalamu kadri itakavyohitajika kwa umma.
Zoezi la utoaji wa chanjo kwa taifa zima linaanza kwa kuihusisha mikoa kumi yenye muingiliano mkubwa wa watu, ambayo ni Dar es Saalam, Mwanza, Mbeya, Arusha, Kigoma, Singida, Dodoma, Iringa, Mtwara na Kilimanjaro ambako kunatajwa kuathirika zaidi katika wimbi hili la tatu.
Hawa Bihoga/DW Dar es Salaam